Jamaa afikishwa mahakamani kwa kutishia 'kukatakata' babake kwa upanga kufuatia mzozo wa urithi Nairobi

Muhtasari

•Mshukiwa anadaiwa kumwambia babake kwa sauti kubwa, "Lazima unipee mali yangu ama nikukatekate!"

•Mahakama ilielekeza kesi hiyo itajwe tena baada ya wiki mbili kwa maelekezo zaidi huku mshukiwa akiachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000.

George Kinyajui katika mahakama ya Kibera
George Kinyajui katika mahakama ya Kibera
Image: CLAUSE MASIKA

Habari na Clause Masika

Jamaa anayedaiwa kutishia kuua babake kufuatia mzozo uliohusisha urithialifikishwa katika mahakama ya Kibera siku ya Jumatatu.

George Kinyajui kutoka Kangemi alikanusha mashtaka dhidi yake mbele ya hakimu Philip Mutua na kuomba kuachiiwa kwa dhamana kidogo.

Kinyajui anatuhumiwa kutishia kuua babake Jenga Kinuthia wakiwa nyumbani kwao katika mtaa wa Kangemi, kaunti ya Nairobi mnamo Septemba 26.

Kulingana na karatasi za mahakama, mlalamishi alikuwa amepumzika  nyumbani kwake wakati ,mshukiwa alifika akiwa amejihami kwa panga.

Inasemekana kwamba mshukiwa alianza kugombeza babake kuhusiana na urithi na kutishia kumuua baada ya kukemewa.

Mshukiwa anadaiwa kumwambia babake kwa sauti kubwa, "Lazima unipee mali yangu ama nikukatekate!"

Inaripotiwa kwamba mshukiwa pia alidai mali ambayo babake aliachiwa na babu yake huku akidai kuwa alitaka kusonga mbele na maisha na kufanya mambo mengine.

Inasemekana kuwa mlalamishi alikimbia kujificha katika duka moja ambako alikaa hadi mwanawe alipoenda ndipo akaenda kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

Mahakama ilielekeza kesi hiyo itajwe tena baada ya wiki mbili kwa maelekezo zaidi huku mshukiwa akiachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000.