Mahakama yakataa kutupilia mbali kesi ya ulaghai dhidi ya mhubiri James Ng'ang'a

Ng'ang'a aliwachiliwa kwa dhamana ya shilingi 500,000.

Muhtasari

•Ng'ang'a alikuwa ameomba kesi hiyo iondolewe akidai kuwa walikuwa wameafikiana  na mlalamishi kupitia barua ya idhini.

•Ng'ang'a anashutumiwa kupokea shilingi 3.6M kutoka kwa mfanyibiashara Wickson Njoroge Mwathi mwaka wa 2016 baada ya kujifanya kuwa angemkodisha jumba lenye vyumba 17 vya kulala katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Image: HISANI

Mahakama imekataa kuondoa kesi ya ulaghai unayohusisha shilingi milioni 3.6 dhidi ya  mhubiri James Ng'ang'a baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kusema kuwa hawajapokea maelekezo ya kuondoa kesi hiyo.

Ng'ang'a alikuwa ameomba kesi hiyo iondolewe akidai kuwa walikuwa wameafikiana  na mlalamishi kupitia barua ya idhini.

"Ningependa kesi iondolewe kwani tumekubaliana kusuluhisha kesi na mlalamishi kupitia barua ya idhini" Mahakama iliambiwa.

Hata hivyo, DPP kupitia kwa wakili Abel Omariba ilipinga wasilisho hilo akidai kuwa hakuwa amepokea maelekezo yoyote ya kuondoa kesi.

Aliomba mahakama kumpatia muda zaidi wa kupitia barua ya idhini na kuipitisha kwa DPP kwa maelekezo zaidi kabla ya kesi hiyo kutupiliwa mbali.

Hakimu mkuu wa Milimani David Ndungi alikubaliana na upande wa mashtaka  huku akisema kuwa DPP ndiye anayeweza kuruhusu kesi hiyo itupiliwe mbali.

Aliagiza mlalamishi kufika mahakamani wakati upande wa mashtaka unaendelea kushauriana na DPP ikiwa kesi itaondolewa  baada ya pande zote kuskizana.

Kesi hiyo itatajwa tena siku ya Ijumaa wiki ijayo.

Ng'ang'a anashutumiwa kupokea shilingi 3.6M kutoka kwa mfanyibiashara Wickson Njoroge Mwathi mwaka wa 2016 baada ya kujifanya kuwa angemkodisha jumba lenye vyumba 17 vya kulala katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Mwezi Juni Mwathi aliambia mahakama kuwa alienda kuona nyumba ile na akaridhika tarehe ambayo hakumbuki vizuri.

Alisema kuwa aliandamana na wakili hadi kwa ofisi za Ng'ang'a mnamo Aprili 2016 ambako walipitia kandarasi pamoja na kutia saini.

Mwathi alisema kwamba alipatia wakili wake pesa ili aende kwenye benki aziweke kwenye akaunti ya Ng'ang'a kwani alikuwa na mkutano mwingine.

Kwa wakati huo upande wa mashtaka ulisema kuwa wakili aliyeweka pesa kwenye akaunti ya Ng'ang'a hakuwa ameandikisha taarifa  na ukaomba aandikishe taarifa kwanza kabla ya kuendelea na kesi.

Wakili wa Ng'ang'a alipinga ombi hilo akisema kuwa kesi ile ilikuwa mzee na upande wa mashtaka ulikuwa na wakati wa kuandikissha taarifa tangu 2016.

Hakimu alikubaliana na upande wa mashtaka na kuamurisha ofisa wa uchunguzi kuchukua taarifa kutoka kwa wakili ambaye aliweka pesa kwenye akaunti ya Ng'ang'a.

Ng'ang'a aliwachiliwa kwa dhamana ya shilingi 500,000.