Majambazi washika familia mateka na kupora mali yao usiku kucha kisha kuibeba kutumia gari lao Nakuru

Muhtasari

•Majambazi hao walijeruhi mzee mwenye nyumba kabla ya kufunga mkewe, bintiye, wajukuu watatu na yaya kwa kamba kisha kuanza kupora mali tofuati kwenye nyumba hiyo usiku kucha.

•Kutia chumvi kwenye jeraha, baada ya kumaliza uporaji wao alfajiri ya kuamkia Jumatano majambazi hao wanadaiwa kupakia mali ambayo walikuwa wamepora kwenye gari la familia aina ya Nissan NV200 na kutoweka kabla ya jua kuchomoza.

crime scene
crime scene

Familia moja kutoka eneo la Bahati, kaunti ya Nakuru inahesabu hasara  baada ya genge la majambazi sita kuvamia nyumba yao usiku wa Jumanne na kuiba mali ya thamani kubwa.

Kulingana na DCI, genge hilo  ambalo lilikuwa limejihami kwa panga lilivamia nyumba ya wahasiriwa mida ya saa tatu usiku wakati walikuwa wanatazaman runinga kabla ya kuelekea kulala.

Majambazi hao walijeruhi mzee mwenye nyumba kabla ya kufunga mkewe, bintiye, wajukuu watatu na yaya kwa kamba kisha kuanza kupora mali tofuati kwenye nyumba hiyo usiku kucha.

Wahalifu hao wanaripotiwa kufanya uporaji wao kwa zaidi ya masaa tisa na kufanikiwa kuiba runinga nne, mitungi mitatu ya gesi, jokofu, kipakatalishi, baiskeli, nguo kati ya vitu vingine.

Baada ya kuridhika na mali ambayo walikuwa wamepora majambazi hao wanasemekana kuhamisha shilingi 80,000 kutoka kwa akaunti ya simu ya binti wa familia na zingine 61,800 kutoka kwa akaunti yake ya benki.

Kutia chumvi kwenye jeraha, baada ya kumaliza uporaji wao alfajiri ya kuamkia Jumatano majambazi hao wanadaiwa kupakia mali ambayo walikuwa wamepora kwenye gari la familia aina ya Nissan NV200 na kutoweka kabla ya jua kuchomoza.

Baada ya masaibu ambayo yalikuwa yamewakumba, familia hiyo iliandamana hadi kituo cha polissi cha Bahati ambapo walipiga ripoti na uchunguzi ukang'oa nanga mara moja.

Wapelelezi waliweza kupata gari ambalo lilikuwa limeibiwa likiwa limeegeshwa kando ya barabara katika eneo la Tuinuane.

Wapelelezi wanaendelea na msako wa majambazi hao huku wahasiriwa wakiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja maeneo hayo.