Jambazi auawa kwa kisu alichokuwa ametia makali akikusudia kutekeleza mashambulizi nacho Kiambu

Muhtasari

•Wanyama ambaye alikuwa amejitolea mhanga kulinda mali yake alikimbilia mkono wa Atuya kwa busara na kumpokonya kisu kisha bila kupoteza muda akamdunga nacho shingoni.

•Atuya alijaribu kuwafuata wenzake huku damu ikiwa inamtoka shingoni  tiriri ila akaanguka na kufariki papo hapo baada ya kupiga hatua chache tu.

crime scene 1
crime scene 1

Jambazi mmoja aliyekuwa amejihami kwa kisu kufanya uhalifu katika eneo la Muguga, kaunti ya Kiambu alipoteza maisha yake baada ya kuwezwa nguvu na mhasiriwa wake mmoja ambaye alimpokonya kisu chake na kukitumia kumuua.

Evans Atuya (35) alikuwa ameandama na majambazi wenzake wawili kushambulia nyumba ya Godwin Wanyama mida ya saa nane usiku wa kuamkia Jumapili bila kufahamu kuwa siku yake ya arubaini ilikuwa imewadia.

Kulingana na DCI, watatu hao walitumia jiwe kubwa kuvunja mlango wa nyumba ya Wanyama ili wapate kuingia ndani kuiba ila mwenye nyumba akaamshwa na kelele zile na hapo kizaazaa kikaanza.

Wanyama ambaye alikuwa amejitolea mhanga kulinda mali yake alikimbilia mkono wa Atuya kwa busara na kumpokonya kisu kisha bila kupoteza muda akamdunga nacho shingoni.

 

Wenzake kuona kilichokuwa kimetendekea mwenzao wakatimua mbio na kutoweka . Atuya alijaribu kuwafuata wenzake huku damu ikiwa inamtoka shingoni  tiriri ila akaanguka na kufariki papo hapo baada ya kupiga hatua chache tu.

Majirani ambao walikuwa wamemshwa na kelele ghasia ambazo zilikuwa zimetokea walijumuika kumsaidia Wanyama ila wakapata alikuwa ashathibiti tukio hilo.

Polisi kutoka kituo cha Muguga walifika katika eneo la tukio na kufanya uchunguzi ili kuthibitisha yalikuwa yametokea.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Gachie huku msako dhidi ya majambazi ambao waliweza kutoroka ukianzishwa.