logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Matamshi ya Junet Mohammed "Baba akishinda serikali ni ya watu wa nyanza" yazua gumzo kubwa

Junet alisikika akihakikishia wakazi wa Nyamira kwamba uongozi utakuwa wa watu wa Nyanza iwapo kinara wa ODM atachukua usukani kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta.

image
na SAMUEL MAINA

Habari23 October 2021 - 10:21

Muhtasari


  • • Junet alisikika akihakikishia wakazi wa Nyamira kwamba uongozi utakuwa wa watu wa Nyanza iwapo kinara wa ODM atachukua usukani kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta.
  • •Junet alimuomba waziri wa afya Mutahi Kagwe  asikasirishwe na matamshi yake huku akidai kwamba eneo alilotoka la Mlima Kenya limekuwa likitawala kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini.
JUNET.jfif

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed amejipata taabani kufuatia matamshi tatanishi ambayo alitoa hadharani siku ya Ijumaa.

Junet amekosolewa sana mitandaoni kuhusiana na madai yake kwamba iwapo  Raila Odinga atanyakua kiti cha Urais kwenye chaguzi kuu za mwaka ujao basi serikali itakuwa mikononi mwa wakazi wa eneo la Nyanza.

Alipokuwa anatoa hotuba yake kwenye hafla ya kuchanga pesa iliyofanyika katika kaunti ya Nyamira ambayo ilikuwa imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwemo Raila Odinga, waziri Fred Matiang'i na Mutahi Kagwe, Junet alisikika akihakikishia wakazi kwamba uongozi utakuwa wao iwapo kinara wa ODM atachukua usukani kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta.

Junet alimuomba waziri wa afya Mutahi Kagwe  asikasirishwe na matamshi yake huku akidai kwamba eneo alilotoka la Mlima Kenya limekuwa likitawala kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini.

"Hapa Nyanza sisi ni watu moja, sisi ni jamii moja. Tusiwe na wasiwasi. Baba akishinda, serikali ni yetu watu wa Nyanza, Sitaki watu wa gazeti wasikie hiyo, Mutahi Kagwe anaweza kasirika, lakini ata nyinyi mlikuwa nayo miaka ishirini na kadharika. Safari hii ni yetu watu wa Nyanza. Mutahi utakuja hapa kama mgeni" Junet alisema.

Matamshi ya mwanasiasa huyo hata hivyo hayajapokewa vyema haswa na wafuasi wa mpinzani mkubwa wa Raila Odinga, naibu rais William Ruto.

Mbunge wa eneo la Soy Caleb Koistany ni miongoni mwa Wakenya waliokuwa katika mstari wa mbele kusuta matamshi ya Junet.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungw'a alisisitiza kwamba Junet alikuwa anazungumza yaliyokuwa moyoni mwake huku akipuuzilia mbali azimio la kinara wa ODM la kuwa rais.

Mamia ya Wakenya wameendelea kutoa hisia mbalimbali mitandaoni wengine wakikemea matamshi ya mbunge huyo huku wengine wakimtetea kwamba yalikuwa ya kitani tu.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved