Rais Uhuru amuomboleza mfanyibiashara Haji Ahmed aliyeaga dunia Jumamosi

Muhtasari
  • Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki wa mwanzilishi wa Dakawou Transporters, Haji Ahmed Nuur Abdulle
Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki wa mwanzilishi wa Dakawou Transporters, Haji Ahmed Nuur Abdulle aliyeaga dunia siku ya Jumamosi.

Katika ujumbe wake wa faraja na kutia moyo, Rais alimsifu Abdulle, 69, kama mjasiriamali na mfadhili bora aliyeanzisha na kuendesha kwa mafanikio kampuni kubwa zaidi ya usafirishaji ya gesi ya Liquefied Petroleum Gas Afrika Mashariki, Dakawou Transporters.

Uhuru alibainisha kuwa kupitia Dakawou Transporters na masuala mengine ya kibiashara, marehemu Abdulle alikuwa ameunda nafasi za kazi kwa maelfu ya vijana wa Kenya.

"Abdulle alikuwa mjasiriamali mnyenyekevu lakini mchapakazi sana ambaye alichangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wetu," alisema.

“Hata tunapoomboleza kifo chake, tunamshukuru Mungu kwa maisha yake yenye matunda mengi hasa ujasiriamali wake uliomwezesha kuchangia pakubwa katika mageuzi ya kiuchumi ya nchi yetu,” Rais alisema.

Abdulle  pia ni mmiliki wa Hospitali ya Premier, mojawapo ya vituo vikubwa vya matibabu vya kibinafsi mjini Mombasa.

Aliomba Mungu aipe familia ya Haji aliyeaga ujasiri na nguvu ya kuomboleza kifo chake.