Shule yafungwa kufuatia ghasia zilizotokea baada ya wanafunzi kukatazwa kutazama mechi kati ya Man U na Liverpool

Muhtasari

•Wanafunzi walijawa na ghadhabu isiyothibitika walipokatazwa kutazama mechi hiyo ambayo iling'oa nanga mwendo wa saa kumi na mbili unusu na wakaharibu mali yenye thamani isiyothibitishwa.

•Walimu walishindwa kuthibiti ghasia hizo na ikabidi waombe usaidizi wa polisi kutoka kituo jirani cha Karatina.

Image: HISANI

Shule ya upili ya wavulana ya Kirimara imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia ghasia ambazo zilijitokeza siku ya Jumapili.

Ghasia kubwa zilishuhudiwa mida ya jioni baada ya usimamizi wa shule hiyo iliyo katika eneo bunge la Mathira kuwanyima wanafunzi ruhusa ya kutazama mechi ya soka kati ya Manchester United na Liverpool.

Wanafunzi walijawa na ghadhabu isiyothibitika walipokatazwa kutazama mechi hiyo ambayo iling'oa nanga mwendo wa saa kumi na mbili unusu na wakaharibu mali yenye thamani isiyothibitishwa.

Walimu walishindwa kuthibiti ghasia hizo na ikabidi waombe usaidizi wa polisi kutoka kituo jirani cha Karatina.

Ghasia hizo zilisababisha kusimamishwa kwa masomo katika shule hiyo kwa kipindi ambacho hakijatambulishwa asubuhi ya Jumatatu.

Kwenye mechi hiyo ambayo ilichezwa ugani Old Trafford mashetani wekundu walinyolewa kichwa bila maji na vijana wa Jurgen Klopp na kucharazwa mabao 5 bila jawabu