Mwanamke achomeka akiokoa mwanawe baada ya mume wake mlevi kuteketeza nyumba kufuatia mzozo wa kinyumbani

Muhtasari

•Diana Mutiso (23) aliugua majeraha mabaya usoni, mikononi na kwenye kiuno alipokuwa anapambana kupenya kwenye moto uliokuwa unaenea kwa kasi  ili kuokoa mtoto wao Olivia (2) .

•Malumbano yalipokuwa yanaendelea Matata anaripotiwa kuchukua chupa yenye mafuta taa na kuyamwaga kote kwa nyumba kisha kuwasha moto na kuacha mkewe na mwanawe wateketee.

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Mwanamke mmoja na mtoto wake walinisurika kifo usiku wa Jumamosi baada ya mumewe kuteketeza nyumba yao wakiwa ndani kufuatia ugomvi wa kinyumbani.

Diana Mutiso (23) alipata majeraha mabaya usoni, mikononi na kwenye kiuno alipokuwa anapambana kupenya kwenye moto uliokuwa unaenea kwa kasi  ili kuokoa mtoto wao Olivia (2) .

Maafisa wa DCI wameripoti kwamba hapo awali David Matata (24) ambaye ni mume wa mhasiriwa alifika nyumbani mwendo wa saa tano usiku akiwa mlevi na kuanza malumbano na mkewe kuhusu suala lisiloeleweka.

Malumbano yalipokuwa yanaendelea Matata anaripotiwa kuchukua chupa yenye mafuta taa na kuyamwaga kote kwa nyumba kisha kuwasha moto na kuacha mkewe na mwanawe wateketee.

Baada ya kuwasha moto ule Matata alitimua mbio na kutoweka huku mkewe akijaribu kumfikia kabla ya kurudi ndani ya nyumba ili kuchukua mwanawe kabla aangamizwe na ukali wa moto ambao ulikuwa umeenea kote.

Mikono ya Diana, kiuno na uso viliugua majeraha mabaya ya moto na kwa sasa anahudumiwa katika hospitali ya Mbooni.

Polisi katika kaunti ya Makueni wanaendelea kumsaka mshukiwa kufuatia matendo yake ya kinyama.