Jamaa kuhudumu kifungo cha miaka 10 kwa kuua mtoto Narok

Muhtasari

•William Kinoti alikuwa amekata rufaa kurekebishwa kwa hukumu hiyo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Narok Francis Gikonyo.

•Mtoto huyo aliuawa mwezi Aprili mwaka wa 2019 katika nyumba yao ya kukodi huko London Estate, mji wa Narok wakati alikuwa anajaribu kutenganisha vita kati ya mhalifu na babake Bw. Edgar Opama.

Mahakama
Mahakama

Mwanamume mwenye umri wa miaka 33 ambaye alikuwa ameshtakiwa kwa mauaji ya msichana wa miaka sita katika eneo la London, Kaunti ya Narok sasa atatumikia kifungo cha miaka 10 baada ya mashtaka yake kupungwa kuwa hatia ya kuua bila kukusudia.

William Kinoti alikuwa amekata rufaa kurekebishwa kwa hukumu hiyo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Narok Francis Gikonyo.

Jaji Gikonyo hata hivyo alitahadharisha kuwa mfungwa huyo hangeweza kuepuka adhabu ya kutozuiliwa, kutokana na uzito wa kosa hilo.

Hii ilikuwa baada ya mahakama kufahamishwa kuwa mfungwa huyo ameelewana na familia ya mwathiriwa baada ya kulipa Sh200, 000.

Mtoto huyo aliuawa mwezi Aprili mwaka wa 2019 katika nyumba yao ya kukodi huko London Estate, mji wa Narok wakati alikuwa anajaribu kutenganisha vita kati ya mhalifu na babake Bw. Edgar Opama.

Mahakama ilisikia kwamba msichana huyo mdogo alimpata Kinoti akiwa amemdunga babake  kisu  usoni na kujaribu kuingilia kati lakini akadungwa shingoni na kufariki papo hapo.

Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilionyesha msichana huyo alikufa kutokana na kuvuja damu kulikosababishwa na kupasuka kwa mshipa wa damu.

Jaji Gikonyo alisema kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba kijana huyo alimuua mtoto huyo kwa kumdunga kisu na kumfunga jela miaka 10.

(Utafsiri: Samuel Maina)