Waziri Eugene Wamalwa awakosoa wandani wa naibu rais William Ruto

Muhtasari

•Wamalwa alisema hamna kipengele cha  katiba kinachowazuia kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii au wafuasi wake.

•Wamalwa amewataka viongozi wa Jamii ya Mulembe kuungana pamoja ili kujipata ndani ya serikali itakayobuniwa mwaka wa 2022 bila kuzingatia misimamo mikali ya kisiasa.

Waziri wa ulinzi nchini Eugene Wamalwa
Waziri wa ulinzi nchini Eugene Wamalwa
Image: LYDIA WAFULA

Waziri wa Ulinzi nchini Eugine Wamalwa amepuuzilia mbali mikakati ya wandani wa naibu wa rais William Ruto ya kuweka muswada wa kuwaondoa madarakani baada ya kuonekana hadharani wakichukua misimamo ya kisiasa licha ya kutoruhusiwa kisheria.

 Akizungumza katika mkutano wa wakulima  eneo la Nzoia,Wamalwa alisema hamna kipengele cha  katiba kinachowazuia kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii au wafuasi wake.

Alisema kuwa katiba ya Kenya inalinda haki ya kila Mkenya kufanya uamuzi wa aina yake, akidai wandani wa Ruto kutaka kuwazuia mawaziri kujihusisha na siasa za nchi ni kinyume cha sheria.

Ni kauli ambayo ilitiliwa mkazo na katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna aliyewataka mawaziri ambao wanakandamizwa na wandani wa Ruto kusimama kidete na kuendelea kupigia debe kiongozi yeyote wa kisiasa.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya  baadhi ya mawaziri katika serikali ya Jubilee kukosolewa vikali na wandani wa Ruto kwa kuchukua msimamo wa kumshabikia kinara wa chama cha ODM Raila Odinga katika kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

 Wakati huo huo Waziri Wamalwa amewataka viongozi wa Jamii ya Mulembe kuungana pamoja ili kujipata ndani ya serikali itakayobuniwa mwaka wa 2022 bila kuzingatia misimamo mikali ya kisiasa.

 Hata hivyo, Waziri Wamalwa alilalamikia pakubwa idadi ndogo ya wakazi wa mkoa wa Magharibi waliojitokeza kujisajili kama wapiga kura kwenye zoezi linaloendelea kote nchini huku akiwarai wale bado ambao hawajasajiliwa kujitokeza na kusajiliwa, akidai kuwa itakuwa vigumu kwa Jamii ya Mulembe iwapo idadi yake ni finyu.