Kesi ya kukomesha mashtaka ya mauaji dhidi ya polisi sita kusikizwa Januari

Muhtasari
  • Kesi ya kukomesha mashtaka ya mauaji dhidi ya polisi sita kusikizwa Januari
Polisi sita ambao walishtakiwa kwa mauaji ya ndugu wawili Embu wakiwa mahakamani
Polisi sita ambao walishtakiwa kwa mauaji ya ndugu wawili Embu wakiwa mahakamani
Image: MAKTABA

Ombi la kutaka kuondoa mashtaka ya mauaji dhidi ya polisi sita wanaoshtakiwa kwa mauaji ya ndugu wawili kutoka Kianjakoma, Kaunti ya Embu litasikizwa Januari mwaka ujao.

Kesi hiyo ilitajwa Jumanne mbele ya Hakimu Daniel Ogembo ambaye aliagiza ombi hilo lisikizwe Januari 25 2022.

Maafisa wa polisi Benson Mputhia, Consolata Kariuki, Nicholas Cheruyoit, Martin Wanyama, Lilian Chemuna na James Mwaniki wamepinga kushtakiwa kwao.

Jaji Ogembo aliwaagiza mawakili wa upande wa utetezi kuwasilisha ombi hilo kwa pande zote kabla ya kesi hiyo kusikizwa.

Maafisa hao waliachiliwa kwa dhamana wiki mbili zilizopita baada ya mahakama kugundua kuwa DPP hakuwa na sababu za msingi za kuwanyima dhamana washtakiwa hao.

Katika maombi yaliyowasilishwa na Wakili Danstan Omari, polisi hao sita wanataka mahakama iamuru uchunguzi ufanyike na kuwafutia mashtaka ya mauaji.

Wamewashtaki Ipoa, DPP na IG, wakisema kuwa kesi hiyoinapaswa kufanyiwa uchunguzi na wala sio kufanyiwa mashtaka

Maafisa hao wanadai kuwa ndugu hao wawili Benson Ndwiga na Emmanuel Ndwiga waliruka kutoka kwa Land Cruiser ya polisi wakati wakitoroka kukamatwa, jambo lililosababisha kifo chao.

Maafisa hao, ambao walikuwa wote katika kituo cha polisi cha Manyatta, kaunti ya Embu, waliambia mahakama kwamba hawafai kushtakiwa kwa mauaji.

Wanasema kuwa mnamo Agosti 1 wakati wa doria za kawaida za polisi na utekelezaji wa amri za kutotoka nje kwa Covid-19, maafisa waliwakamata jumla ya washukiwa 10, kati yao ndugu.

Maafisa hao wamesema waligundua kuwa ndugu hao wawili hawakupatikana walipofika kituo cha polisi cha Manyatta na mmoja wa washukiwa akawaambia aliwaona wawili hao wakiruka nje ya gari.

Walikuwa wakisafirishwa katika kituo cha polisi na gari la  Land Cruiser GKB 277 T.

"Washukiwa hao walikuwa wakipandishwa pamoja kwenye gari moja la polisi, watu waliofariki katika kitendo cha kujitoa mhanga wakati wakitoroka chini ya ulinzi halali waliruka nje ya gari la polisi lililokuwa likitembea hivyo kufariki dunia," nyaraka za mahakama zilisema.