Jamaa ahukumiwa kifungo cha maisha kwa kunajisi mtoto Siaya

Muhtasari

•Katika ushahidi wake, mwathiriwa aliiambia mahakama kuwa mnamo tarehe 18 Novemba 2019, mshtakiwa alimshawishi waandamane hadi nyumbani kwake baada ya kumnunulia ndizi.

•Baada ya kutenda aibu hiyo  mshtakiwa alimuonya mhasiriwa asimfichulie yeyote kilichokuwa kimetendeka.

Mahakama
Mahakama

Mahakama kuu ya Siaya imemhukumu mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 35 amehukumiwa  kifungo cha maisha kwa kunajisi msichana wa miaka minne.

Simon Oduor Oloo alishtakiwa kwa kutenda kosa hilo mnamo Novemba 18, 2019 katika kijiji cha Malanga katika kaunti ndogo ya Gem.

Katika ushahidi wake, mwathiriwa aliiambia mahakama kuwa mnamo tarehe 18 Novemba 2019, mshtakiwa alimshawishi waandamane hadi nyumbani kwake baada ya kumnunulia ndizi.

Oduor aliambia msichana huyo kwamba alitaka wawe marafiki na baada ya hapo akamwelekeza ajiunge naye kitandani kisha akamnajisi.

Mmoja wa mashahidi wa upande wa mashtaka alieleza mahakama  kuwa wakati alikuwa anacheza na rafiki yake, mwathiriwa alikwenda na kumweleza kuwa ‘Bier’( kama alivyojulikana mshtakiwa), alikuwa amemnunulia mandazi na ndizi kisha kumnajisi nyumbani kwake wakati mama yake hakuwa karibu.

Baada ya kutenda aibu hiyo  mshtakiwa alimuonya mhasiriwa asimfichulie yeyote kilichokuwa kimetendeka.

 Shahidi huyo alimfahamisha mamake mwathiriwa ambaye mnamo tarehe 20 Novemba 2019, aliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Yala baada ya kumhoji binti yake zaidi.

Msichana huyo mdogo baadaye alipelekwa hospitalini kwa uchunguzi ambao ulithibitisha kuwa alikuwa amenajisiwa.

Mamake mwathiriwa, Violet Atieno, aliambia mahakama kwamba bintiye alifichua kuwa ilikuwa mara ya pili kwa mshtakiwa kumnajisi na kwamba mara ya kwanza, mshtakiwa alimvuta kwa ndizi.

Kutokana na hayo, mama ya mhasiriwa aliomba mahakama imhukumu mshtakiwa kifungo cha kukaa chini ya ulinzi kwa kuwa alihofia angeweza kudhulumu mtoto mwingine.

Hata hivyo, mshtakiwa alipofika mbele ya Hakimu Muthoni Mwangi, alikana mashtaka akidai alikuwa akihangaishwa na mama ya mwathiriwa kwa madai ya masuala ya ardhi.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Muthoni Mwangi, alibainisha kuwa mshtakiwa alikuwa na sifa mbaya kutoka kwa jamii na anaripotiwa kuwa mtu wa jeuri.

Pia alibainisha kuwa kesi za unajisi zimekithiri katika jamii na anatumai kuwa kifungo cha maisha kinachotolewa kitapeleka ujumbe mzito kwa watu wengine katika jamii ili kuwaepusha wahalifu wa uhalifu huo kuwafanyia watoto ukatili huo.

(Utafsiri: Samuel Maina)