Rais Ramaphosa aishukuru Kenya kwa uungwaji mkono wakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi

Muhtasari
  • Rais Ramaphosa aishukuru Kenya kwa uungwaji mkono wakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi
  • Rais wa Afrika Kusini alizungumza Jumanne jioni mjini Pretoria alipoandaa karamu ya kitaifa kwa heshima ya Rais Uhuru Kenyatta
Rais Cyril Ramaphosa
Image: PSCU

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameishukuru Kenya kwa kuunga mkono vita vya nchi yake vya kupigania uhuru kutoka kwa ubaguzi wa rangi.

"Kenya ilitoa usaidizi usioyumba na mshikamano kwa miaka mingi wakati wa mapambano yetu dhidi ya mfumo mbovu wa ubaguzi wa rangi," Rais Ramaphosa alisema.

Rais wa Afrika Kusini alizungumza Jumanne jioni mjini Pretoria alipoandaa karamu ya kitaifa kwa heshima ya Rais Uhuru Kenyatta na ujumbe wake.

Rais Ramaphosa alidokeza kuwa Ziara ya Kiserikali ya Rais Kenyatta imewezesha nchi hizo mbili kufanya upya ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kuweka msingi thabiti wa ushirikiano zaidi kati ya jumuiya za wafanyabiashara wa mataifa hayo mawili ya kiuchumi barani Afrika.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kenyatta alisisitiza dhamira ya Kenya ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Afrika Kusini kwa manufaa ya watu wa nchi hizo mbili.

Rais Kenyatta alibainisha kuwa Kenya na Afrika Kusini zimefurahia uhusiano wa kidiplomasia wa joto na mzuri ambao ulianza wakati ambapo ubaguzi wa rangi ulikomeshwa mwaka wa 1994, akiongeza kuwa nchi hizo mbili zinashiriki maadili ya msingi ambayo yanaunganisha watu wao pamoja.

"Uhusiano wetu kati ya watu na biashara na uwekezaji kati ya mataifa yetu mawili yenye undugu umestawi na ninaamini baada ya ziara hii, hata watainuka zaidi.

Ni hamu yangu kubwa kuona uhusiano huu wa kudumu kati ya mataifa yetu mawili ukiimarika zaidi katika miaka ijayo," Rais Kenyatta alisema.

Katika vita dhidi ya Covid-19, Rais Kenyatta alipongeza juhudi kubwa za Rais Ramaphosa katika kukabiliana na janga hilo nchini Afrika Kusini na katika bara la Afrika kwa ujumla.