Jamaa 40, akamatwa kwa kunajisi msichana wa darasa la 7 Homabay

Muhtasari

•Joshua Ochieng Arum 40, alikamatwa alipokuwa akijaribu kuafikiana na familia ya mhasiriwa ili kutupilia mbali kosa hilo.

•Mama ya mhasiriwa Everline Akoth alisema aliona mabadiliko fulani kwa bintiye aliporudi kutoka msituni na kumhoji.

•Inadaiwa kuwa kituo cha afya pamoja na wazazi wa msichana huyo walipanga njama ya kuficha ukweli na wakati wanakijiji walipata taarifa kuhusu njama hiyo wakaghadhabika na kuwafahamisha polisi.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Mashariki wanamzuilia mwanamume mmoja ambaye anadaiwa kumnajisi msichana wa miaka saba Jumatatu alasiri katika kijiji cha Kanyasare, eneo ndogo la Kakelo Kamroth.

Joshua Ochieng Arum 40, alikamatwa alipokuwa akijaribu kuafikiana na familia ya mhasiriwa ili kutupilia mbali kosa hilo.

Inaripotiwa mtoto huyo alikuwa ameenda kukusanya kuni pamoja na watoto wengine wakati Arum alimvamia na kufanya kitendo hicho cha kinyama huku watoto wengine wakisimama kutazama.

Mama ya mhasiriwa Everline Akoth alisema aliona mabadiliko fulani kwa bintiye aliporudi kutoka msituni na kumhoji.

"Binti yangu alirudi akitembea bila raha kana kwamba anaumwa na nguo zake zimechafuka," Akoth alibainisha.

Baada ya kumhoji bintiye, mama huyo alikuja kujua masaibu yaliyotokea kule msituni.

Akoth pia alieleza kuwa jirani yake pia alifika nyumbani kwake na kumfahamisha kuhusu tukio hilo msituni, akisema kwamba watoto wengine walioshuhudia kitendo hicho walimweleza siri.

Mtoto huyo alikimbizwa katika Kituo cha afya cha Manga kabla ya kupewa rufaa hadi Hospitali ya Rachuonyo Kusini iliyoko Oyugis ambako alitibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani.

Kulingana na maelezo ya matibabu yaliyoonekana na waandishi wa habari, daktari alithibitisha vyema kwamba ilikuwa kesi ya unajisi.

Inadaiwa kuwa kituo cha afya pamoja na wazazi wa msichana huyo walipanga njama ya kuficha ukweli na wakati wanakijiji walipata taarifa kuhusu njama hiyo wakaghadhabika na kuwafahamisha polisi.

Akithibitisha kisa hicho, Chifu Msaidizi wa eneo hilo Tom Ondiro alisema alimhoji mtoto huyo na kubaini mshukiwa alikuwa akimnajisi huku akiongeza  kuwa kisa cha hivi punde ni mara ya tatu.

Mshukiwa anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Ringa katika Kaunti Ndogo ya Rachuonyo akisubiri kufikishwa mahakamani.

(Utafsiri: Samuel Maina)