MC Jessy ajiunga na chama cha UDA,afichua kiti atakachowania

Muhtasari
  • Mcheshi huyo alithibitisha Jumatano kwamba amejiunga rasmi na chama kinachoongozwa na DP William Ruto baada ya mashauriano mapana
  • MC Jessy alisema DP alimpigia simu na kumwalika kwenye chama cha UDA
MC Jessy na Naibu Rais William Ruto
Image: MC Jessy/INSTAGRAM

Mchekeshaji wa kipindi cha Churchill Jasper Muthomi, almaarufu Mc Jessy, atawania kiti cha ubunge cha Imenti Kusini kwa tiketi ya chama cha UDA.

Mcheshi huyo alithibitisha Jumatano kwamba amejiunga rasmi na chama kinachoongozwa na DP William Ruto baada ya mashauriano mapana.

MC Jessy alisema DP alimpigia simu na kumwalika kwenye chama cha UDA.

"Sasa ni wazi maono yanaelekea wapi. Baada ya siku nyingi za mikutano ya mashauriano na watu wangu wa Imenti Kusini, nimealikwa rasmi kujiunga na UDA," alisema.

Aliongeza kuwa hangeweza kukataa kujiunga na UDA kwa sababu ndiko watu wake wanataka awe mwanachama.

"Kazi ya msingi ambayo imefanywa hatimaye imefikia upande wa timu iliyoshinda. Nilipopokea simu kutoka kwa mkuu Hustler Kunialika, ilibidi nisikilize wito wangu wa Watu na wito wake wa kujiunga na Timu iliyoshinda. Na kazi ya kufafanua upya Imenti ya Kusini Sasa ianze."