Ruto awaomboleza wawaniaji wawili wa UDA walioaga dunia

Muhtasari
  • Polisi walisema alikuwa akisafiri kwa matatu iliyokuwa ikielekea Nairobi ilipogongana na basi
Image: DP Ruto/TWITTER

Chama cha United Democratic Alliance kilipata pigo chini ya saa 24 baada ya wawaniaji wake wawili kufariki katika ajali mbili tofauti za barabarani.

Mgombea ubunge wa eneo bunge la Nandi Hills Wesley Kibet Kogos na mwenzake wa Wadi ya Chaania Nancy Wanjala Mwashuma walifariki katika ajali za barabarani Nairobi na Mombasa mtawalia.

Kiongozi wa chama cha UDA Naibu Rais William Ruto amejutia vifo vyao katika risala ya rambirambi iliyotumwa kwa familia na wawakilishi wa viongozi hao wawili.

"Tunaomba Mungu azifariji familia zao na wapiga kura. Familia ya UDA inasimama nao katika nyakati hizi ngumu," DP aliandika.

Kogo alikuwa wa kwanza kupoteza maisha katika ajali iliyotokea Alhamisi asubuhi huko Kangemi, Nairobi, alipokuwa akielekea kwenye studio za Kass FM kwa mahojiano.

Polisi walisema alikuwa akisafiri kwa matatu iliyokuwa ikielekea Nairobi ilipogongana na basi.

Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa 5.30 asubuhi.

Mkuu wa trafiki wa polisi Nairobi Joshua Omukata alisema wanachunguza kisa hicho.

"Ni yeye pekee aliyekufa wakati huo. Hatukujua alikuwa mgombeaji,” alisema Omukata.

Mwashuma kwa upande mwingine alifariki alipokuwa akielekea kwenye maziko ya kaka yake yanayotarajiwa Jumamosi, Aprili 9.

Ajali hiyo ya Ijumaa asubuhi ilitokea Voi eneo la Ngutunyi kando ya Barabara kuu ya Mombasa- Nairobi.

Wawili hao walikumbana na vifo vyao wiki moja tu kabla ya uteuzi wa chama cha UDA utakaoandaliwa kote nchini Aprili 15.