Familia ya mfanyikazi aliyechemka hadi kifo katika kiwanda cha chuma kupokea 7,000 kila mwezi

Muhtasari

•Mnamo Alhamisi familia ilisema kwamba mmiliki wa Blue Nile Rolling Mills aliiambia familia kuwa hiyo itakuwa "ishara ifaayo ya fidia."

•Marehemu aliburutwa kwenye kinu cha kusaga chuma mnamo Machi 25, na kupondwa vipande-vipande kabla ya mwili wake kuanguka kwenye tanuru ya moto.

Marehemu Calleb Otieno
Marehemu Calleb Otieno
Image: HAND OUT

Familia ya Caleb Otieno, mwanamume aliyeyeyuka hadikuwa  jivu katika kiwanda cha chuma cha Thika, itapewa marupurupu ya kila mwezi ya Sh7,000 kwa miaka mitano kama fidia na kampuni hiyo.

Hii ni thuluthi moja ya mshahara wake wa kila mwezi wa Sh21,000. Aliajiriwa kwa masharti ya kudumu na alikuwa amefanya kazi kwa miaka saba.

Hii ni tafsiri ya mkupuo wa Sh420,000 ambao ulikuwa umeonyeshwa na ripoti za vyombo vya habari.

Mnamo Alhamisi familia ilisema kwamba mmiliki wa Blue Nile Rolling Mills aliiambia familia kuwa hiyo itakuwa "ishara ifaayo ya fidia."

Michael Orao, binamu yake ambaye amekuwa akizungumza na wanahabari kwa niaba ya familia, alisema  kwamba kampuni hiyo ilimpa babake Otieno Sh100,000 mnamo Machi 27 familia ilipotembelea kiwanda hicho.

Pesa hizo ziliwasaidia kumudu gharama za malazi na usafiri.

Orao alisema,bosi wa kiwanda hicho  alisema kuanzia hapo, atamchukulia baba yake Otieno kama mmoja wa wafanyakazi wake na angepokea posho kama mfanyakazi mwingine yeyote kwenye orodha ya malipo.

Orao alisema kampuni hiyo ilielekeza familia kufuata fidia "ya maana" kutoka kwa kampuni ya bima.

"Mhindi anayemiliki kampuni hiyo ndiye aliyependekeza mawazo hayo na kuamua peke yake bila kupokea  maoni yoyote. Nadhani waliona jinsi mzee alivyokuwa maskini na wakaamua kutoa kiasi hicho cha kejeli," Orao alisema.

"Walileta hoja ya fidia wakati familia ilikuwa bado imeguswa na kifo. Mtazamo wetu ulikuwa kwenye kifo tu lakini walichagua kuja bado kukiwa na moto."

Marehemu ambaye alikuwa na umri wa miaka 34 alitokea kijiji cha Kogony, kaunti ya Kisumu. Aliburutwa kwenye kinu cha kusaga chuma mnamo Machi 25, na kupondwa vipande-vipande kabla ya mwili wake kuanguka kwenye tanuru ya moto.

Wadadisi wa masuala ya kisheria wanasema  familia ya marehemu inafaa kutafuta wakili wa majeraha ya kibinafsi ili kuwatetea dhidi ya kampuni na mashirika ya bima katika kutafuta fidia.

Wadadisi wanasema kwamba mjadala kuhusu fidia lazima uzingatie umri wa kuishi unaowezekana wa mfanyakazi na kwamba hesabu inapaswa kujumuisha salio la maisha ambayo mhasiriwa angeweza kufanya kazi.

Mzozo huo umefichua hitaji la Wakenya kuwa na ufahamu zaidi wa haki zao iwapo watajeruhiwa au kufa wakiwa kazini.

(Utafsiri: Samuel Maina)