Waiguru aomba msamaha baada ya kutaja Azimio katika hafla ya Kenya Kwanza

Muhtasari
  • Waiguru aomba msamaha baada ya kutaja Azimio katika hafla ya Kenya Kwanza

Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru mnamo Jumatatu, Aprili 11, aliomba msamaha kwa Naibu Rais, William Ruto, kutokana na makosa aliyofanya alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya Kenya Kwanza.

Akizungumza katika uwanja wa Ngong Racecourse, ambapo vyama viliambatanisha rasmi saini zao ili kujiunga na Kenya Kwanza, Waiguru alimtaja Ruto kuwa kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja.

Bosi huyo wa Kaunti ya Kirinyaga alisitisha hotuba yake mara moja ili kuomba msamaha kwa DP ambaye pia ni mgombeaji urais wa United Democratic Alliance (UDA).

"Mheshimiwa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya na kiongozi wa chama cha UDA na kiongozi wa muungano wa Azimio...," Waiguru alishtuka, kabla ya kusimamisha hotuba yake

Pole sana, Mungu wangu!.... Na kiongozi wa muungano wa Kenya Kwanza. Samahani kwa dhati, kwa sababu nilikuwa nikifikiria nitakachosema kuwahusu," aliomba msamaha huku akiendelea na hotuba yake.

Tukio hilo lilizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii huku wakosoaji wake wakipendekeza kuwa tukio hilo ni ushahidi kwamba moyo wake bado unaweza kuwa Azimio.