Afisa wa GSU avamiwa na majambazi akielekea kujiburudisha na wanawake wawili

Muhtasari

•Mhasiriwa alivamiwa katika eneo la Mihang'o  wakati alipokuwa anarudi kambini kutoka eneo la burudani.

•Afisa yule aliwageukia washukiwa kwa ngumi na mateke huku akijeruhi mmoja wao vibaya na kumuacha bila meno matatu.

Crime scene
Crime scene

Wapelelezi jijini Nairobi wanawasaka majambazi wawili ambao walimvamia afisa wa GSU na kumuwacha na majeraha mwilini.

Mhasiriwa ambaye ni mkufunzi katika shule ya mafunzo ya GSU alivamiwa katika eneo la Mihang'o usiku wa kuamkia Alhamisi wakati alipokuwa anarudi kambini kutoka eneo la burudani.

Kitengo cha DCI kimeripoti kwamba mhasiriwa alikuwa ameandamana na wanadada wawili wakati washukiwa waliposhambulia na kukatiza sherehe yao ghafla

Punde baada ya mashambulizi yale, wanadada wale walitoroka njia tofauti na kumuacha mhasiriwa akimenyana na wavamizi wale.

Afisa yule aliwageukia washukiwa kwa ngumi na mateke huku akijeruhi mmoja wao vibaya na kumuacha bila meno matatu.

Mshukiwa wa pili kuona vile alitoa kisu alichokuwa ameficha na kumdunga mhasiriwa.

Kwa hofu ya kuangamizwa, afisa huyo aligura eneo la tukio na kuenda kuwaita wenzake ili wamsaidie kukabiliana na majambazi hao.

Hata hivyo washukiwa walifanikiwa kutoroka kabla ya maafisa zaidi kutua katika eneo la tukio. 

Meno matatu ya mshukiwa mmoja na nywele aina ya wig ambazo ziliachwa nyuma na wanadada waliokuwa na mshukiwa zilipatikana pale.

Mhasiriwa alikimbizwa katika hospitali ya Ruai huku uchunguzi zaidi na msako wa washukiwa uking'oa nanga.