Jamaa wawili matatani kwa kuiba na kuchinja ng'ombe wa jirani yao Kilifi

Muhtasari

•Wawili hao kutoka kijiji cha Kitsonga wanaripotiwa kuiba ng'ombe wa Bw Hamisi Mwakazidi siku ya Alhamisi kisha kumchinja.

•Majirani na polisi walifanya upekuzi wa kina nyumbani kwa jirani huyo na kupata mzoga wa ng'ombe ukiwa umekwa ndani ya magunia.

Jamaa wawili watiwa mbaroni kwa kuiba na kuchinja ng'ombe wa jirani
Jamaa wawili watiwa mbaroni kwa kuiba na kuchinja ng'ombe wa jirani
Image: FACEBOOK// NPS

Wanaume wawili wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Tiwi, kaunti ya Kwale kwa madai ya kuiba ng'ombe wa jirani yao.

Wawili hao kutoka kijiji cha Kitsonga wanaripotiwa kuiba ng'ombe wa Bw Hamisi Mwakazidi siku ya Alhamisi kisha kumchinja.

Polisi wameripoti kuwa Bw Mwakazidi aliamka Alhamisi asubuhi na kupata ng'ombe wake akiwa ametoweka kutoka zizini.

Punde baada ya kugundua n wake hayupo alikusanya marafiki kadhaa ambao walimsaidia kufuata nyayo za mnyama huyo ambazo zilielekea nyumbani kwa jirani yake mmoja.

Jirani huyo alitoweka baada ya kuona kundi la watu nyumbani kwake na kumuacha rafiki yake Hamisi Ndegwa ambaye alishindwa kueleza alichokuwa anafanya pale.

Kufuatia hayo majirani na polisi kutoka kituo cha Tiwi walifanya upekuzi wa kina nyumbani kwa jirani huyo na kupata mzoga wa ng'ombe ukiwa umekwa ndani ya magunia.

Bw Mwakazidi alitambua mzoga huo kuwa wa ng'ombe wake ambaye alikuwa ameibiwa na hapo jirani huyo pamoja na rafikiye wakatiwa pingu.

Wawili hao wanaendelea kuzuiliwa huku wakisubiri kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la wizi.