Jamaa taabani kwa kuua mkewe na kumzika kisiri Nandi

Muhtasari

• Naftali Avendi, 59, alikamatwa  baada yake kuthibitisha kuwa mpenzi wake, 30, alifariki na akamzika nyumbani kwake.

•Avendi aliwapeleka polisi mahali ambapo alimzika mkewe katika kijiji cha Kamoron, eneo la Kabwareng-Nandi kusini.

Crime scene
Crime scene

Polisi katika eneo la Kobujoi, kaunti ya Nandi wanamzuilia mwanamume mmoja anayeshukiwa kumuua mpenziwe na kuzika mwili wake kisiri.

Mkuu wa polisi wa Nandi Kusini John Owuoth alisema mshukiwa, Naftali Avendi, 59, alikamatwa  baada yake kuthibitisha kuwa mpenzi wake, 30, alifariki na akamzika nyumbani kwake.

"Majirani wake katika kijiji cha Kamoron walishuku kwamba jambo lisilo la kawaida huenda limetokeabaada ya mwanamke huyo kutoweka na mshukiwa alipohojiwa alikiri kwamba mkewe alikufa na akamzika kisiri," Owuoth alisema.

Avendi aliwapeleka polisi mpaka mahali ambapo alimzika mkewe katika kijiji cha Kamoron, eneo la Kabwareng-Nandi kusini.

"Tunaelekea mahakamani leo kuomba amri ya kutaka mwili wa marehemu ufukuliwe ili uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake." OCPD alifichua.

Kupitia  mahojiano ya simu Jumatatu alasiri, bosi huyo wa polisi alisema maafisa wa upelelezi wanaamini kuwa marehemu aliuawa

Polisi walikuwa wakimtafuta mwanafamilia wa karibu wa marehemu kabla ya kutaja jina lake. Hata hivyo, maafisa kutoka DCI walitarajiwa kuwasilisha ombi lao mahakamani Jumatatu alasiri.

Owuoth alitoa wito kwa umma kuwa waangalifu zaidi na kuhakikisha kuwa jamaa zao wanajulikana walipo kila mara.

“Katika enzi hii ya visa vingi vya kujitoa uhai na mauaji, lazima tuwe macho, Owuoth aliongeza.

(Utafsiri: Samuel Maina)