Watu 20 walazwa hospitalini baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani Nakuru

Muhtasari

•Wahudumu wa St John’s Ambulance waliwapatia majeruhihao Huduma ya Kwanza kabla ya kuwakimbiza hospitalini kwa matibabu zaidi.

•Haya yalitokea saa chache baada ya watu 7 kufariki kwenye ajali mbaya ya barabarani kwenye barabara ya Narok-Bomet.

Image: ST JOHNS AMBULANCE

Watu 20 walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Naivasha Ijumaa jioni baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Kinugu, kando ya barabara kuu ya Nakuru-Nairobi.

Wahudumu wa St John’s Ambulance waliwapatia majeruhihao Huduma ya Kwanza kabla ya kuwakimbiza hospitalini kwa matibabu zaidi.

Ajali hiyo ilihusisha Lori, Matatu ya abiria 14  na gari la kibinafsi.

Haya yalitokea saa chache baada ya watu 7 kufariki kwenye ajali mbaya ya barabarani kwenye barabara ya Narok-Bomet.

Ajali hiyo ilitokea Ijumaa mwendo wa saa sita adhuhuri katika eneo la Silanka.

Ilihusisha matatu ya Ena Coach  iliyokuwa ikielekea Nairobi na trela iliyokuwa inaelekea Bomet.

Dereva wa trela alikuwa akiendesha gari kutoka Narok kuelekea upande wa Bomet na alipofika eneo la ajali, guruduma la mbele upande wa kulia likapasuka.

"Alipoteza udhibiti wa trela na kugonga Matatu iliyokuwa ikielekea upande huo  mwingine. Kutokana na ajali hiyo, matatu ya PSV iliharibika vibaya na kusababisha vifo na majeruhi," kamanda wa kaunti ndogo ya Narok Kaskazini Alphonce Shiundu alisema.

Watano walifariki papo hapo huku wengine wawili wakifariki kutokana na majeraha walipokuwa wakipokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Narok.

Miili ya watu 7 waliofariki imehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Narok.

"Watano kati ya walionusurika wanapokea matibabu katika hospitali moja," alisema.

Watu wengine watano waliohusika katika ajali hiyo wanapokea matibabu hospitalini baada ya kupata majeraha.

Wengi wa waliojeruhiwa walipata majeraha ya kichwa na mikono.