"Maisha yamekuwa safari ya upweke sana bila wewe!" Sonko anamkumbuka marehemu babake kihisia

Muhtasari

•Babake Sonko alifariki mnamo Septemba 15, 2015 katika hospitali ya Nairobi baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.

•Sonko alisema kila Father's Day humkumbusha nyakati ambazo babake alikuwa hai na wangeweza kusherehekea pamoja.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: HISANI

Jumapili dunia yote iliadhimisha siku ya kina baba duniani.

Walimwengu walitumia fursa hiyo kuwasherehekea kina baba maalum katika maisha yao huku wengine wakiwakumbuka walioaga.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko hakuachwa nyuma huku akitumia siku hiyo maalum kumkumbuka marehemu baba yake Gideon Kioko Mbuvi.

Sonko alisema kila Father's Day humkumbusha nyakati ambazo mzazi huyo wake alikuwa hai na wangeweza kusherehekea pamoja.

"Kila Siku ya kina baba kawaida hunirudisha katika siku bora zaidi za maisha yangu nilipoisherehekea siku hii na wewe. Ingawa hauko tena hapa na sisi, ninajisikia vibaya na mwenye huzuni kwamba siwezi kukukumbatia ili kukutakia Siku njema ya akina baba," Sonko aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mgombea huyo wa ugavana wa Mombasa alikiri kuwa maisha yake hayajakuwa sawa tangu kifo cha baba yake.

"Bila wewe, maisha yamekuwa safari ya upweke sana kusema  kweli lakini asante baba kwa kuniacha na kumbukumbu nzuri za kuthamini," Alisema.

Babake Sonko alifariki mnamo Septemba 15, 2015 katika hospitali ya Nairobi baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.

Bw Kioko Mbuvi alifariki akiwa na umri wa miaka 67. Wakati huo Sonko alikuwa anahudumu kama seneta wa Nairobi.

Takriban miongo miwili kabla ya kifo cha babake mwanasiasa huyo alimpungia mamake mkono wa buriani.

Bi Saumu Mukami Mbuvi alifariki mnamo Desemba 2, 1997 na kuzikwa nyumbani kwao katika eneo la Pwani.

Kila mwaka Sonko amekuwa akitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuadhimisha siku ambayo mamake alifariki.

Desemba iliyopita gavana huyo wa zamani aliadhimisha miaka 24 tangu mamake alipofariki na kueleza kuwa bado huwa anaumia kila anapomkumbuka.

"Ni miaka 24 sasa tangu ulipoenda kuwa na Mungu. Nashukuru Mungu kwa muda ambao alitupa sisi watoto wako kukujua na kukupenda. Maisha yako yalinifanya kile nilicho leo na kifo chako kikanifanya kuhisi uchungu wa watu wengine wanaoumia na kuteseka. Machozi ya siri bado hutiririka tunapokufikiria. Kuishi bila wewe ni karibu haiwezekani. Ulipokuwa hai tulikupenda na hata baada ya kufa tunakupenda. Tunashukuru Mungu kwa kuruhusu tuwe sehemu ya maisha yako. Tunajua bado uko nasi  ukituangalia. Kuenda kwako kulibadili maisha yetu kabisa na kutufanya tukupende zaidi" Sonko alisema kupitia Facebook.