Ushuru kwenye Gesi ya kupika yapunguzwa

Upungufu huo mkubwa unakuja mwaka mmoja baada ya Bunge kurejesha VAT

Muhtasari

•Hazina imepunguza ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) unaotozwa kwa gesi ya kupikia kwa nusu, na kuwapa watumiaji afueni kubwa kutokana na kupanda kwa bei ya kimataifa ya bidhaa hiyo na bidhaa nyingine za petroli.

GESI
GESI
Image: FILE STAR

Hazina imepunguza ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) unaotozwa kwa gesi ya kupikia kwa nusu, na kuwapa watumiaji afueni kubwa kutokana na kupanda kwa bei ya kimataifa ya bidhaa hiyo na bidhaa nyingine za petroli.

Sheria ya Fedha ya 2022 ilipunguza ushuru wa usambazaji wa gesi ya petroli (LPG) kutoka asilimia kumi na sita ya sasa hadi asilimia nane.

Upungufu huo mkubwa unakuja mwaka mmoja baada ya Bunge kurejesha VAT ya asilimia kumi na sita kwenye gesi ya kupikia.

Kupunguzwa kwa VAT kwenye LPG  zinaonyesha wazi juhudi zinazoendeshwa na  Serikali kufanya bidhaa hiyo kuwa nafuu kwa wakenya.

Serikali inapanga kufufua mpango wa kusambaza  vifaa vya LPG kuanzia Julai mwaka huu. Baadhi ya mitungi 60,000 ya LPG ya kilo sita imepangwa kusambazwa.

Wizara ya Petroli tayari imekaribisha zabuni za usambazaji wa mita za kisasa (smart meters) zitakazowekwa kwenye mitungi itakayosambazwa miongoni mwa wa Kenya  wenye  kipato cha chini nchini.

Utekelezaji wa mpango huo hata hivyo ulitatizwa na baadhi ya wasambazaji ambao walitoa mitungi zenye hitilafu.

Mpango huo pia uliathiriwa vibaya na changamoto za usambazaji katika Shirika la Taifa la Mafuta linalomilikiwa na Serikali ambalo lilifa kuendesha programu hiyo.