Mwanamke akimbia baada ya kumtupa mtoto mchanga kwenye choo

Aliongeza kuwa shimo hilo lina kina cha futi 15.

Muhtasari

•Wakaazi wa kituo cha biashara cha Mururi kaunti ya Kirinyaga waliamka na hali ya kushangaza Jumapili, Julai 10, 2022, baada ya kugundua mtoto mchanga ametupwa kwenye choo cha shimo.

•Kulingana na chifu wa lokesheni ya Kirimara Naftaly Gichimu, mtoto huyo aligunduliwa na mwanamume aliyekuwa ameenda chooni, na baada ya kuingia alisikia kilio cha mtoto mchanga.

Mama akiwa amemshika mtoto.
Mama akiwa amemshika mtoto.
Image: FACEBOOK

Wakaazi wa kituo cha biashara cha Mururi kaunti ya Kirinyaga waliamka na hali ya kushangaza Jumapili, Julai 10, 2022, baada ya kugundua mtoto mchanga ametupwa kwenye choo cha shimo.

Kulingana na chifu wa lokesheni ya Kirimara Naftaly Gichimu, mtoto huyo aligunduliwa na mwanamume aliyekuwa ameenda chooni, na baada ya kuingia alisikia kilio cha mtoto mchanga.

Mtu huyo alifahamisha umma mara moja ambao walimjulisha chifu kuhusu suala hilo.

Baada ya hapo, wananchi waliungana mkono na kumuokoa mtoto huyo akiwa hai.

Mtoto huyo wa kike baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Kimbimbi katika wadi ya Nyangati Kaunti Ndogo ya Mwea Mashariki ambako anaendelea na matibabu.

"Nilipokea simu kutoka kwa mkazi wa eneo la Mururi ambaye aliniambia kuwa mtoto mchanga alisikika akilia kutoka kwenye choo cha shimo ndani ya kituo cha maduka," chifu wa eneo hilo alisema.

Aliongeza kuwa shimo hilo lina kina cha futi 15.

Wakazi walilaani kitendo hicho wakikitaja kuwa ni cha kinyama.

"Inasikitisha sana mwanamke kujifungua na kumtupa mtoto asiye na hatia kwenye shimo na kuacha mtoto kufa," alisema mkazi mmoja aliyetambulika kwa jina la Wambura.

Kitendo hicho kilikashiwa vibaya  sana, umaskini mbaya au gharama kubwa ya maisha haipaswi kuwa kisingizio cha kutekeleza kitendo kama hicho.

"Watu wanapaswa kuwajibika kwa matendo yao. Ukizaa unapaswa kuwa tayari kumlea mtoto. Afadhali uombe usaidizi kutoka kwa watu wengine badala ya kusababisha hili," aliongeza.

Sasa wanataka uchunguzi ufanyike ili kumkamata mama huyo ambaye bado haijulikani mahali aliko.