Mchimbaji ambaye mwili wake ulipatikana miezi 8 baada ya ajali ya mgodi hatimaye azikwa

Mabaki ya Okwach yalipatikana mapema mwezi baada ya msako wa miezi minane.

Muhtasari

•Marehemu alizikwa hai wakati akifanya kazi katika migodi ya Abimbo katika kaunti ndogo ya Bondo na mwili wake kukosekana.

•Mama wa marehemu alisimulia mateso ambayo familia ilipitia katika kipindi cha miezi minane iliyopita huku akitokwa na machozi

Shughuli za uokoaji katika ajali ya mgodi wa dhahabu wa Abimbo huko Bondo, kaunti ya Siaya
Shughuli za uokoaji katika ajali ya mgodi wa dhahabu wa Abimbo huko Bondo, kaunti ya Siaya
Image: DICKENS WESONGA

Mwili wa Tom Okwach, mmoja wa waathiriwa wa ajali ya mgodi wa dhahabu iliyotokea Desemba mwaka jana hatimaye umezikwa. 

Marehemu alifunikwa akiwa hai wakati akifanya kazi katika migodi ya Abimbo katika kaunti ndogo ya Bondo lakini harakati za kuondoa mwili wake zikakosa kufua dafu.

Mabaki ya Okwach hata hivyo  yalipatikana mapema mwezi huu kutoka migodini baada ya sakasaka za miezi minane.  

Hatimaye alizikwa Jumatano nyumbani kwake katika eneo la Abimbo. 

Mnamo Disemba 2 mwaka jana, wachimba migodi wanane akiwemo Okwach walinaswa ndani ya mgodi wenye kina cha futi 500 baada ya mgodi huo kuporomoka wakiwa ndani, na kuwazika wakiwa hai kwa siku kadhaa. 

Kufuatia shughuli za uokoaji zilizofanywa na kikosi maalum cha maafisa wa serikali za kitaifa na zile za kaunti, watu sita kati yao waliokolewa wakiwa hai, huku mchimba mgodi mmoja akipatikana amekufa baada ya wiki moja ya juhudi za uokoaji. 

Shughuli za uokoaji zilisimamishwa baada ya wiki mbili za msako wakati ilionekana kuwa mchimbaji mgodi aliyekuwa amesalia, Okwach, angeweza kuwa amekufa. 

Lakini kwa sababu ya mila na imani za Wajaluo familia ya Okwach haikuweza kumuacha mmoja wao na ilibidi wakite kambi kwenye eneo hilo kwa zaidi ya miezi 7, huku wakiwatumia wachimbaji wa mikono kutafuta mwili.

Wananchi kutoka sehemu mbalimbali za kaunti ya Siaya walijaa kwenye ibada ya mazishi ili kumpungia mkono mchimbaji huyo aliyenaswa kwa miezi kadhaa akiwa amezikwa chini zaidi ya futi 500 kwenye ardhi. 

Wazazi wa Okwach ambao walimsifu mtoto wao kama mtu mchapakazi aliyejitolea kuhudumia familia yake, walifichua jinsi jamaa na marafiki walivyowashinikiza kuacha msako huo na badala yake wazike shina la ndizi kwa kufuata mila za Wajaluo, lakini wakasisitiza kusubiri. mwili wa mtoto wao kupatikana.

Mama wa marehemu alisimulia mateso ambayo familia ilipitia katika kipindi cha miezi minane iliyopita huku akitokwa na machozi, huku watu wengi wakiwataja kwa majina na kuwalaumu kwa kifo cha mtoto wao na kushindwa kwa wapekuzi kupata mabaki yake.            

Hata hivyo walitoa shukrani kwa jamaa na marafiki na utawala wa eneo hilo ambao ulisimama nao katika wakati wao mgumu.            

Mjane wa Okwach, Jacklyne Okwach, 23, alisimulia jinsi baba wa watoto wake wawili aliondoka nyumbani siku hiyo ya maafa, na kurudishwa nyumbani kwa mazishi miezi minane baadaye.

Alisema kwamba alifurahi kumzika mumewe nyumbani kwake na kuweka nyuma taabu za kutafuta mwili wake kwa muda mrefu.

Viongozi wa kisiasa wakiongozwa na mwaniaji MCA wa wadi ya Sakwa Kusini Eunice Ndolo waliomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuwekeza zaidi katika kujitayarisha kwa majanga na kusaidia wachimba migodi katika eneo hilo kuhusu masuala ya usalama ili kuepusha vifo kama hivyo visivyotarajiwa.

(Utafsiri: Samuel Maina)