logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Miguna azungumzia suala la kurejea Kenya baada ya Ruto kutwaa urais

Wakili huyo amedokeza kuhusu kurejea kwake hivi karibuni.

image
na SAMUEL MAINA

Habari16 August 2022 - 06:36

Muhtasari


  • •Miguna alifurushwa Kenya kufuatia  jukumu lake katika uapisho usio rasmi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kama "rais wa wananchi"
  • •Amebainisha kuwa atarejea nchini baada tu Ruto kuapishwa kama rais wa tano wa nchi na tahadhari nyekundu zilizotolewa dhidi yake kuondolewa.
Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018

Wakili maarufu aliyefukuzwa  nchini Miguna Miguna amedokeza kuhusu kurejea kwake hivi karibuni.

Miguna alihamia Kanada Februari 2018 baada ya kufurushwa nchini kufuatia mashtaka ya makosa yanayohusiana na uhaini. Masaibu yaliyomkumba yalifuatia jukumu lake katika uapisho usio rasmi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kama "rais wa wananchi"

Wakili huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiikosoa serekali  ya Kenya pamoja na washirika wake sasa amedai kuwa tayari amepanga virago vyake kwa ajili ya maandalizi ya kurejea nchini. 

"Kwa wazalendo wote, Tulieni. Asanteni kwa mshikamano. Ndiyo, nimefunga virago na niko tayari," Alisema.

Miguna alitoa tangazo hilo kupitia Twitter muda mfupi baada ya Ruto kutangazwa kuwa mshindi wa kinyang'anyiro cha urais cha mwaka huu.

Baadhi ya Wakenya hasa wanaouunga mkono muungano wa Kenya Kwanza walikuwa wamemshinikiza wakili kurejea nchini kufuatia ushindi wa Ruto.

Miguna hata hivyo amebainisha kuwa atarejea nchini baada tu ya kiongozi wa Kenya Kwanza kuapishwa kama rais wa tano wa nchi na tahadhari nyekundu zilizotolewa dhidi yake kuondolewa.

"Nitawaona hivi karibuni. Cheers," Alisema.

Takriban miezi mitano iliyopita Miguna alimuidhinisha Ruto kuwa rais wa tano wa Kenya hadharani. 

Katika mahojiano na Look Up Tv, Wakili huyo alidai kwamba amekuwa akishurutishwa kumuidhinisha mwajiri wake wa zamani Raila Odinga  ila ameshikilia msimamo wake kuwa hakuna uwezekano wake kumuunga mkono tena.

"Siwezi kumuunga mkono Raila Odinga. Leo nikiwa kwenye runinga ya taifa namuidhinisha William Ruto 100% na naomba Wakenya wote tumpigie kura," Miguna alisema.

Miguna amekuwa mkosoaji sugu wa utawala wa rais Uhuru Kenyatta tangu alipofurushwa kutoka Kenya miaka minne iliyopita.

Mzozo wake na serikali ulizuka alipomwapisha Raila Odinga kama rais wa Kenya katika uwanja wa Uhuru Park baada ya uchaguzi wa 2017.

Baba huyo wa watoto watatu pia hajakuwa na uhusiano mwema na kinara wa ODM tangu alipokubali kufanya kazi na rais. Mapema mwaka huu Miguna aliapa kuuza mali yake yote na kukana uraia wa ke wa Kenya iwapo Raila atashinda katika uchaguzi ujao.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved