Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Maseno kaunti ya Kisumu alifariki siku ya Ijumaa baada ya kuanguka kutoka kwa bweni.
Mkurugenzi wa Elimu Kanda ya Nyanza Nelson Sifuna alithibitisha kisa hicho, akisema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini ni nini kilichosababisha kifo cha kijana huyo.
Mvulana huyo alianguka kutoka ghorofa ya pili ya bweni katika shule hiyo, Sifuna alisema.
"Tumepokea ripoti kwamba mwanafunzi huyo aliacha barua ya kujiua. Ninataka polisi kuchunguza tuhuma hizo,” aliongeza mkuu huyo wa elimu wa mkoa.
Mwili wa kijana huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Aga Khan mjini Kisumu.
Kwingineko ni kuwa Watu watatu, akiwemo mwanafunzi, walifariki Ijumaa asubuhi, Agosti 26, baada ya lori kugonga basi la shule katika Soko la Ntharene huko Imenti Kusini, Kaunti ya Meru.
Basi hilo lililokuwa likielekea eneo la Kanyakine lilikuwa likisafirisha wanafunzi kuwapeleka shuleni wakati lori lililokuwa likielekea Nkubu lilipoteza mwelekeo na kusababisha ajali hiyo.
Watu watatu, madereva wawili na mwanafunzi walikufa papo hapo. Wanafunzi zaidi ya kumi walijeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Consolata, Nkubu.
Miili ya madereva na mwanafunzi huyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.