Mwanamke afariki katika ajali wakati akimkimbiza mumewe na mpango wake wa kando

Marehemu alimpata mumewe na mwanamke mwingine katika duka moja jijini Calabar.

Muhtasari

•Marehemu anaripotiwa kupoteza uhai baada ya gari lake kupoteza mwelekeo na kuingia kichakani kando ya barabara kuu ya Murtala Mohammed.

•Mwanamke huyo alikimbizwa hospitalini lakini kwa bahati mbaya akafariki kutokana na majeraha mabaya aliyopata.

Gari lililohusika katika ajali
Image: FACEBOOK// STEPHEN OKPOSIN

Mwanamke mmoja kutoka Nigeria alifariki baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani wakati alipokuwa akiwafuata mumewe na mpango wake wa kando baada ya kuwapata pamoja katika duka moja jimboni Cross River.

Tukio hilo lilitokea Jumapili katika mji wa Calabar, Kikosi cha Usalama wa Barabarani cha Shirikisho nchini Nigeria  (FRSC) kimethibitisha.

Marehemu anaripotiwa kupoteza uhai baada ya gari lake kupoteza mwelekeo na kuingia kichakani kando ya barabara kuu ya Murtala Mohammed.

Kulingana na shahidi wa ajali hiyo, mume wa marehemu aliendesha gari lake kwa kasi baada ya kumuona na mwanamke huyo akaamua kumfuata nyuma.

"Nilikuwa naendesha nyuma yao na chini ya dakika tatu nilimwona akihusika kwenye ajali na alikuwa amepoteza fahamu hadi kiwango cha kufa," Stephen Okposin ambaye alishuhudia ajali hiyo alisema.

Okposin alisema mume wa mwanamke huyo alikimbia katika eneo la tukio kumsaidia baada ya kumshusha mpango wake wa kando.

Mwanamke huyo alikimbizwa hospitalini lakini kwa bahati mbaya akafariki kutokana na majeraha mabaya aliyopata.

Akithibitisha tukio hilo Jumapili usiku, kamanda wa polisi wa Nigeria alisema ajali hiyo ilisababishwa na mwendo kasi.