Mshtuko baada ya mwili wa mtoto mchanga kupatikana kwenye shimo la takataka

"Tunashuku maiti hiyo iliangushwa na mama ambaye hakutaka kumlea mtoto wake," mkaazi alisema.

Muhtasari

•Jomo alisema mwili huo ulikuwa umefunikwa na kipande cha kitambaa na ulikuwa bado haujaoza wakati ulipogunduliwa.

•Kamanda wa Polisi wa Narok Central Frederick Shiundu alisema wanachunguza kisa hicho ili kubaini ni nani aliyetupa mwili huo.

crime scene
crime scene

Wakaazi wa eneo la Total katika kaunti ya Narok wamekumbwa na mshtuko baada ya mwili wa mtoto wa miezi tisa kupatikana ukiwa umetupwa kwenye shimo la takataka.

Mwenyekiti wa Nyumba Kumi katika eneo hilo, Jacob Jomo alisema alipata taarifa kutoka kwa wakazi kuwa kulikuwa na mwili ambao ulikuwa umelazwa kwenye eneo la kutupa na baada ya kufika pale, aliwapata watu kadhaa wakiwa wamekusanyika kushuhudia.

Jomo alisema mwili huo ulikuwa umefunikwa na kipande cha kitambaa na ulikuwa bado haujaoza wakati ulipogunduliwa.

“Matukio kama haya yanazidi kuwa ya kawaida katika eneo hili. Tunashuku kuwa maiti hiyo iliangushwa na mama ambaye hakutaka kumlea mtoto wake. Tunawasihi wasichana wetu kutoshiriki mapenzi bila kinga ikiwa hawako tayari kulea watoto,” alisema.

Naye Antony Mintilla, mkazi aliyeshuhudia tukio hilo, aliwataka wanawake wanaojifungua watoto bila mpangilio kuomba msaada kutoka kwa mamlaka kama vile ofisi za watoto, makao ya watoto au makanisani ili wapate mwongozo wa kulea watoto wao.

"Inasikitisha kwamba mtu anajifungua mtoto mwenye afya njema na kushindwa kuwalinda ilhali tuna familia nyingi ambazo hazijajaliwa watoto," alisema.

Kamanda wa Polisi wa Narok Central Frederick Shiundu alisema wanachunguza kisa hicho ili kubaini ni nani aliyetupa mwili huo kwenye shimo la mbolea na sababu za kitendo hicho kiovu.

Alitoa wito kwa wakazi kutoa taarifa zozote zitakazopelekea kukamatwa kwa mhalifu akisema kila maisha ni ya thamani sana na takatifu.

Shiundu alimtaka mtu yeyote ambaye anapata changamoto katika kulea watoto wake kuomba mwongozo ofisini kwake, na kuongeza kuwa wapo maofisa waliohitimu mafunzo wanaoshughulikia masuala ya jinsia.

"Si lazima uteseke peke yako kwa ukimya kiasi cha kumuua mtoto wako, unaweza kutembelea ofisi yetu na kuelezea changamoto zako na kwa pamoja tunaweza kusaidia kutatua shida," alisema.