Jumanne, mwanamume mwenye umri wa miaka 42 alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na mahakama ya Murang’a baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanamke kiziwi na mwenye matatizo ya kiakili.
Hakimu mkuu Peter Maina alisema mshtakiwa Samuel Gachau alikuwa na hatia ya kosa alilotenda mnamo Desemba 31, 2021.
Gachau alishtakiwa kwa kutekeleza uhalifu huo wa kingono katika kijiji kimoja cha eneo la Gatui, Kaunti ya Murang’a.
Kulingana na mashahidi waliofikishwa mahakamani, mshtakiwa alitumia fursa ya changamoto ya kimwili na kiakili ya mlalamikaji kumnyanyasa kingono.
Dada ya mlalamishi aliambia mahakama kuwa dadake alikuwa shambani wakati mshtakiwa alipomvizia na kumbaka.
“Dada yangu hasikii wala kuongea vizuri na mara nyingi anapenda kwenda shambani kuangalia na kucheza na nyani na kama kawaida yake alikuwa shambani, nilimsikia akipiga kelele nikaenda kumuokoa, nilimkuta hana nguo na amejilaza. chini,” shahidi huyo alisimulia mbele ya mahakama.
Aidha alisema mshtakiwa alikamatwa na wananchi baada ya kuitana. "Niliwapigia simu wenyeji ambao walisaidia kumkamata Gachau na baadaye akapelekwa katika kituo cha polisi cha Murang'a," alisema.
Ripoti ya kimatibabu iliyowasilishwa kortini ilionyesha kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa na matatizo ya kiakili na kwa hakika alidhulumiwa kingono katika tarehe iliyotajwa.
Jitihada za mshtakiwa za kutaka kesi hiyo ifutwe na kumaliza mzozo wao nje ya mahakama ilishindikana baada ya Hakimu kusema kosa hilo ni kubwa.
Katika kujitetea kwake, mshtakiwa aliomba ahurumiwe akisema ana matatizo ya kifua. Alipewa siku 14 kukata rufaa iwapo hakuridhika na hukumu hiyo.
Utafsiri: Samuel Maina