Majonzi ! Mzee akifariki baada ya kushambuliwa na nyuki Nyeri

Polisi walitaja tukio hilo kuwa la kusikitisha na wanafanya uchunguzi.

Muhtasari

•Mwili wa Joseph Waweru Gichohi ulipatikana ukiwa ndani ya boma lake mnamo Jumamosi, muda mfupi baada ya kushambuliwa.

•Haijabainika ni nini kilichochea nyuki hao kusababisha shambulio hilo lililotokea mwendo wa saa tisa mchana.

Rip
Rip
Image: HISANI

Mwanamume mwenye umri wa miaka 80 alipatikana amefariki baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki katika kijiji cha Thunguma, Kaunti ya Nyeri.

Mwili wa Joseph Waweru Gichohi ulipatikana ukiwa ndani ya boma lake mnamo Jumamosi, Desemba 3, 2022 muda mfupi baada ya kushambuliwa.

Polisi walitaja tukio hilo kuwa la kusikitisha na wanafanya uchunguzi.

Walioshuhudia walisema mwili wa marehemu ulikuwa umelala ukitazama juu huku nyuki wengi wakiwa wameufunika.

Hakukuwa na mtu mwingine ndani ya boma hilo. Hata kuku na mbwa walikuwa wameepuka hasira ya wadudu hao.

Haijabainika ni nini kilichochea nyuki hao kusababisha shambulio hilo lililotokea mwendo wa saa tisa mchana.

Polisi waliitwa kwenye eneo la tukio na kuuhamisha mwili huo hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Outspan kusubiri zoezi la uchunguzi wa maiti.

Polisi walisema wanakusudia kufungua uchunguzi ili kubaini jinsi na kwa nini alikufa.

"Hatuwezi kudhania sisi wenyewe kwamba alikufa kutokana na kuumwa na nyuki. Hilo litaamuliwa kupitia uchunguzi na uchunguzi wa maiti utaeleza zaidi,” afisa mkuu anayefahamu kisa hicho alisema.