Wakenya kwenye mtandao wa Twitter, almaarufu KOT ni watu wenye ubunivu wa aina yake ikija ni masuala ya kuwapa majina ya majazi watu maarufu nchini.
Hivi karibuni baada ya binti wa kwanza wa rais William Ruto kuonekana katika ziara mbali mbali nchini, Wakenya kwenye Twitter waliibuka na jina la majazi ambalo sasa limeonekana kutumiwa sana kumzumzia Charlene Ruto.
Quickmart Ivanka, ndilo jina ambalo amekuwa akihusishwa nalo haswa baada ya kuonekana akifanya ununuzi katika tawi moja la duka la jumla, Quickmart.
Lakini ni je, unajua jina hili liliasisiwa kwake kwa nini?
Ivanka ni binti wa kwanza wa Rais wa 45 wa Marekani Donald Trump, alikuwa makamu wa rais mtendaji wa Shirika la Trump linalomilikiwa na familia na aliwahi kuwa jaji wa baraza katika kipindi cha televisheni cha baba yake. Mnamo Machi 2017, alikua mshauri mkuu wa utawala wa rais wa baba yake.
Ivanka alionekana akijishughulisha pakubwa na mambo mbalimbali mwanzoni mwa uongozi wa babake kama rais mpaka ikafikia muda akapewa wadhifa serikalini.
Wakenya walifananisha kujishughulisha kwa Ivanka na kule kwa Charlene ambaye amekuwa na ziara katika sehemu nyingi nchini kutoa hamasisho kwa vijana kuhusu mkopo wa Hustler Fund miongoni mwa mengine – jambo ambalo limeibua kumbukumbu vichwani mwa Wakenya kama zile za mtoto wa rais Trump.
Charlene alipewa jina la utani baada ya kuhusika kwake mara kwa mara katika biashara ya serikali katika nafasi isiyojulikana.
Miongoni mwa wengine ambao wamevuna majina ya majazi kutoka kwa KOT ni rais Ruto ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiitwa Doyen na hivi majuzi jina la Nabii limeasisiwa kwa ajili yake, naibu rais Rigathi Gachagua anayeitwa Riggy G, spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula anayeitwa Papa wa Roma miongoni mwa wengine.