Wakatoliki wa Kiafrika wanahitaji uwakilishi zaidi -kasisi

Aliongeza kuwa hakuna makadinali wa Kiafrika wanaoshikilia afisi zozote kuu katika kanisa hilo

Muhtasari

•“Sisi Waafrika lazima tuwe mezani. Afrika ina Wakatoliki milioni 236 – kanisa linalokuwa kwa kasi zaidi duniani,” Padre Stan Chu Ilo aliambia podikasti ya BBC Africa Daily.

•"Papa anafikiri, na mimi pia nina hakika, kwamba tunapaswa kuzingatia jinsi tungejenga kanisa na jamii yetu kwenye mabega ya vijana hawa," aliongeza.

Image: BBC

Kabla ya ziara ya Papa Francis nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hivi leo makasisi wa Nigeria wamesema kunahitajika uwakilishi zaidi wa Waafrika katika Kanisa la Katoliki.

“Sisi Waafrika lazima tuwe mezani. Afrika ina Wakatoliki milioni 236 – kanisa linalokuwa kwa kasi zaidi duniani,” Padre Stan Chu Ilo aliambia podikasti ya BBC Africa Daily.

Aliongeza kuwa hakuna makadinali wa Kiafrika wanaoshikilia afisi zozote kuu katika kanisa hilo.

Katika mahojiano pamoja na Dada Rosemary Nyirumbe, mtawa wa Uganda ambaye anajulikana kama ‘Mama Teresa wa Afrika’, Padre Stan aliongeza kuwa Papa anataka Afrika iwe na sauti.

"Sijawahi kumuona Papa Francis akiwa na uchangamfu kama vile nilivyomwona kwenye mazungumzo haya ya mtandaoni kati ya vijana wapatao 3,000 wa Kiafrika," alisema.

"Papa anafikiri, na mimi pia nina hakika, kwamba tunapaswa kuzingatia jinsi tungejenga kanisa na jamii yetu kwenye mabega ya vijana hawa," aliongeza.

Dada Rosemary pia alisema kuwa Papa anakuja wakati muhimu kwa sababu anaweza "kuleta mtazamo wa matumaini kwa watu" ambao wamekabiliwa na shida kwa "muda mrefu".

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sasa inakabiliwa na mzozo unaoongezeka mashariki mwa nchi hiyo unaochochewa na makundi ya watu wenye silaha.

Papa pia atazuru Sudan Kusini ambayo imekuwa ikikabiliwa na migogoro kwa miaka mingi.