Mamake Jeff Mwathi azirai katika ofisi za DCI huku familia akitafuta haki

Babake Jeff alikuwa akihutubia wanahabari wakati mkewe alipoanguka nyuma yake.

Muhtasari

•Babake Jeff alikuwa akielezea kutamaushwa kwake na mfumo wa haki wa nchi wakati mkewe alipozirai.

•Bw Ngugi alisikitika jinsi haki kwa mwanawe ilivyochukua muda mrefu kupatikana.

alizari katika ofisi za DCI siku ya Jumanne, Machi 14.
Mamake Jeff Mwathi alizari katika ofisi za DCI siku ya Jumanne, Machi 14.
Image: HISANI

Mama ya marehemu Geoffrey Mwathi almaarufu Jeff, Hannah Wacuka, alizimia nje ya makao makuu ya DCI, kando ya Barabara ya Kiambu wakati familia ilipokuwa ikihutubia waandishi wa habari siku ya Jumanne.

Babake Jeff, Bw Peter Ngugi alikuwa akielezea kutamaushwa kwake na mfumo wa haki wa nchi wakati mkewe alipozidiwa na hisia, akaangua kilio na kuanguka chini kabla ya kuondolewa katike eneo hilo.

"Sisi tunataka haki na tujue ni kwa nini wale walimuua. Walimuua kwa sababu gani na walikuwa wanataka nini. Hilo pekee ndilo tunaomba. Ni jambo ambalo tungetaka lishughulikiwe kwa haraka," Bw Ngugi aliwaambia wana habari huku mkewe ambaye alikuwa amesimama nyuma yake akiendelea kulia.

Bw Ngugi alisikitika jinsi haki kwa mwanawe ilivyochukua muda mrefu kupatikana na kuhoji kwa nini waliomuua bado hawajakamatwa.

"Kwa nini wale walihusika na kifo cha Jeff hadi wa leo hawajakamatwa? Hilo ndilo swali tunauliza kama familia," Bw Ngugi alisema kabla ya kumgeukia mke wake ambaye alikuwa akiomboleza ili kumfariji.

Alimwacha nyanyake Jeff, Bi Teresia Nyokabi aendelee kuwahutubia wanahabari huku akiendelea kumfariji mkewe. Ni wakati nyanyake Jeff alipokuwa akizungumza ambapo Bi Wacuka alianguka nyuma yake.

"Mimi nashindwa hii kesi inaendelea namna gani. Waharakishe hii maneno ndio angalau ata sisi familia tuwe watulivu kwa roho zetu. Kwa sababu sasa unaona vile kuko. Nataka DCI wajaribu kuharakisha," alisema wakati mama Jeff alipoanguka.

Bi Nyokabi alisema kuwa familia haijapokea ripoti yoyote kutoka kwa wapelelezi tangu Jeff alipofariki mnamo Februari 22. Alibainisha kuwa familia itapata amani tu baada ya haki kupatikana na washukiwa kukamatwa.

Jeff Mwathi aliaga dunia mwezi uliopita chini ya mazingira tatanishi na Wakenya wameendela kutoa shinikizo kubwa kwa wapelelezi kuhakikisha kwamba haki ya kijana huyo wa miaka 23 imepatikana.

Marehemu alikuwa nyumbani kwa mwimbaji wa nyimbo za Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo wakati alipodaiwa kuanguka kutoka kwa orofa ya kumi na kukumbana na kifo chake cha uchungu.