Kwa mara ya kwanza, baada ya Zaidi ya miezi miwili, kiongozi wa upinzani Raila Odinga amemtambua William Ruto kama rais mteule wa Kenya, baada ya kukataa kumtambua hivyo mara kadhaa.
Katika mahojiano ya kipekee katika runinga ya TV 47 usiku wa Jumamosi, Odinga alimrejelea Ruto kama rais wakati alikuwa anasema kwamba katika maandamano yao, watawasilisha ujumbe wao kwake ikuluni.
"Tutawasilisha malalamishi yetu kwa Rais William Ruto," Raila Odinga alisema.
Kwa wafuatiliaji wakuu wa hotuba za Odinga tangu kukamilika kwa uchaguzi, hii ndio mara ya kwanza kwake kumtambua Ruto kama rais.
Mnamo Januari 24, 2023, kiongozi huyo wa upinzani nchini Kenya aliwaambia maelfu ya wafuasi wake katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi kwamba hamtambui William Ruto kama rais wa nchi.
Odinga pia alidai uchaguzi wa urais mnamo Agosti 2022 uliibiwa dhidi yake.
"Hatuwezi na hatutatambua serikali ya Kenya Kwanza na kufikiria serikali yake kuwa haramu," Odinga alisema.
"Sisi kama Azimio tunakataa matokeo ya uchaguzi wa 2022. Hatuwezi na hatutatambua utawala wa Kenya Kwanza na kuchukulia serikali ya Kenya Kwanza kuwa haramu. Hatumtambui William Ruto kama Rais wa Kenya,” Odinga alisema.
Odinga hata hivyo alisisitiza kwamba maandamano yake dhidi ya serikali ya Ruto yataendelea vile yalivyoratibiwa licha ya mkuu wa polisi kanda ya Nairobi, Adamson Bungei kuharamisha maandamano hayo.
Odinga katika mahojiano hayo alisema kwamba wafuasi wake hawataandamana kwa wingi kwenda ikuluni bali watawatuma wawakilishi wachache, wawili au watatu kuwasilisha ujumbe wao kwa rais Ruto.
Hata hivyo, vyombo vya usalama vimebaki na msimamo wao kwamba maeneo ya karibu na ikulu ya Nairobi yanasalia kuwa marufuku kukaribiwa na mtu yeyote ambaye hana idhini ya kukaribia makazi hayo ya rais.