logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Idadi ya maiti zilizofukuliwa Shakahola imepita 200 huku zaidi ya watu 600 wakiendelea kutafutwa!

Hata hivyo, jitihada za kutafuta na kuokoa zinaendelea.

image
na Davis Ojiambo

Habari14 May 2023 - 08:46

Muhtasari


  • • Kamishna wa eneo la pwani alisema watu 610 mpaka sasa wameripotiwa kutojulikana waliko na familia zao.
  • • Aliongeza kuwa sampuli 93 za DNA zimekusanywa na kwamba waathiriwa 14 wameunganishwa tena na familia zao.

Shughuli ya ufukuzi wa maiti katika kaunti ya Kilifi shamba la Shakahola la mchungaji mwenye itikadi potovu Paul Mackenzie ilirejelewa mapema wiki jana na mpaka sasa idadi ya maiti zilizofukuliwa kijumla imepita 200.

Kufikia Jumamosi jioni, maafisa wa DCI wanaoendesha shughuli hiyo katika shamba lenye ukubwa wa ekari 800 walifukua maiti 22 zaidi na kufanay idadi hiyo kuzidi 200.

Idadi hiyo inaendelea kunenepa mithili ya puto linalopuliziwa hewa ndani yake kila uchao huku familia nyingi zikiwa zimekita kambi eneo hilo wakiwa na Imani ya kupata wapendwa wao waliotoweka nyumbani wakidaiwa kujiunga na kanisa la Mackenzie miaka michache iliyopita.

Baada ya kufukuliwa kwa miili 22 zaidi Jumamosi, kamishna wa eneo la Pwani Rhoda Onyancha alisema kwamba mtu mwingine mmoja anayeshukiwa kuwa mwanachama wa Mackenzie alitiwa mbaroni na kufichua kwamba taarifa walizo nazo ni kuwa takribani watu 610 wameripotiwa kutojulikana waliko huku shughuli hiyo ikiendelea.

Aliongeza kuwa sampuli 93 za DNA zimekusanywa na kwamba waathiriwa 14 wameunganishwa tena na familia zao.

Onyancha pia alisema ili kupanga upya usaidizi huo wa vifaa, ufukuaji huo ulikuwa umesitishwa kwa siku mbili, kuanzia Jumapili, Mei 12, hadi Jumanne, Mei 16. Hata hivyo, jitihada za kutafuta na kuokoa zinaendelea.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved