Msanii wa Kenya, Thomas Kiptanui Kemboi almaarufu Kapkeno amekuwa akivuma mitandaoni katika kipindi cha siku chache zilizopita baada ya kulazwa hospitalini kwa kula mayai 15 ili kutimiza ahadi yake ya kula trei ya mayai iwapo klabu ya Manchester United ingechapwa na Arsenal.
Kapkeno alikuwa ameonyesha imani kubwa kuwa klabu yake anayoipenda zaidi ya Manchester United ingeshinda dhidi ya Arsenal katika uwanja wa Emirates Jumapili iliyopita na hata akaapa kula mayai 30 iwapo washindi hao wa kombe la Carabao msimu uliopita wangeshindwa. Hayawi hayawi basi huwa, kufikia mwisho wa dakika 90 pamoja na muda wa nyongeza za mchuano huo mjini London, matokeo yalikuwa Arsenal 3- Manchester United 1, kumaanisha kwamba Kapkeno alikuwa amepoteza dau lake na ilimbidi ale mayai yale.
Msanii huyo kutoka Eldoret baadaye alijaribu kutimiza ahadi yake huku marafiki zake wawili wakitazama na kupeperusha tukio zima moja kwa moja kwenye mtandao wa Facebook. Hata hivyo, alipokuwa amekula nusu ya trei, alionekana kupata matatizo na akazimia.
Marafiki zake ambao mwanzoni walidhani anatania walimpeleka hospitalini ambapo aligundulika kuwa ana tatizo la kuvimbiwa na kulazwa.
Kapkeno hata hivyo si mtu wa kwanza kuweka dau la kushangazwa kwenye mechi ya soka. Wafahamu wengine;
2. Arap Uria
Mwezi Machi, mtayarishaji wa maudhui Arap Uria alianza safari ya baiskeli kutoka mji wa Eldoret hadi Nairobi City baada ya timu yake anayoipenda, Chelsea kushindwa na Manchester United.
Uria alikuwa ameahidi kufanya safari hiyo ya takriban kilomita 311 kwa baiskeli ikiwa Man United ingewashinda The Blues kwenye uwanja wa Old Trafford.
Bahati mbaya kwake, mechi hiyo iliisha kwa Mashetani Wekundu kushinda mabao 4-1, hivyo basi ikabidi afanye safari yake.
3. Mchekeshaji Gogo Small
Mwezi Machi, mchekeshaji wa Eldoret 'Gogo Small' ambaye pia ni shabiki sugu wa Manchester United alilazimika kutembea nusu uchi katika mitaa ya mji huo wa kaunti ya Uasin Gishu baada ya kuahidi kufanya hivyo ikiwa timu yake anayopenda zaidi ingeshindwa na Liverpool katika mechi yao ya EPL.
Ili kutimiza ahadi yake, mchekeshaji huyo alivua nguo zake akabaki nusu uchi na kupiga filimbi alipokuwa akitembea barabarani baada ya Liverpool kuwalaza mashetani wekundu 7-0. Alibaki na pampers tu baada ya kuvua nguo zingine.
4. Stanley Amani na Tonny Shilla
Mwaka wa 2018, wanaume wawili kutoka Tanzania, Stanley Amani na Tonny Shilla walifanya makubaliano ya maandishi ambapo waliapa kuwasalimisha wake zao kwa wiki nzima ikiwa Manchester United au Manchester City wangeshindwa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.
Amani alisema katika makubaliano hayo kwamba rafiki yake Shilla angemchukua mke wake ikiwa Manchester City haingeshinda. Shilla, kwa upande wake, alikubali kupeana mke wake kwa muda kama huo endapo Manchester United ingeshindwa.
5. Binod Kumar Shah
Mwanamume wa Kihindi, Binod Kumar Shah , pia aliwekelea dau la mke wake mnamo Novemba 2019 na akamshambulia vibaya wakati alipokataa kwenda.