Waziri wa maendeleo ya viwanda na biashara Moses Kuria amefichua kwamba Wakenya wanaolia kuhusu kupandishwa kwa bei ya mafuta usiku wa kuamkia Septemba 15 na mamlaka ya EPRA watazidi kulia hata Zaidi mpaka Februari mwakani.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kuria alisema kwamba wanaolia kuwa bei ya mafuta imepanda wafahamu kuwa huo ndio mwanzo tu kwani bei hizo zitazidi kuongezeka kwa kiwango kisichopungua shilingi 10 kila mwezi.
Kuria alisema kuwa bei za mafuta zimekuwa ghali si tu nchini Kenya pekee bali ni kote ulimwenguni na ifikapo mwezi Februari mwakani, bei ya mafuta ya petroli ambayo imevuka shilingi mia mbili kwa lita kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, itakuwa inauzwa kwa Zaidi ya shilingi 270.
Bei Ghafi Ulimwenguni ziko kwenye mteremko wa juu. Kwa madhumuni ya kupanga tarajia bei ya pampu kupanda kwa Ksh 10 kila mwezi hadi Februari,” Kuria alitweet.
Baada ya bei mpya, Petroli sasa imeanza kuuzwa kwa sh211.64 kutoka bei ya awali ya sh194.68, na Dizel itauzwa kwa sh200.99 kutoka kwa bei ya mwezi jana ya sh179.67 huku mafuta ya taa yakiuzwa sh202.61 kutoka kwa bei ya mwezi Agosti ya sh169.48 jijini Nairobi.
EPRA, katika taarifa kwa vyumba vya habari Alhamisi usiku, ilifichua kuwa bei ya Super Petrol sasa imeongezeka kwa Ksh.16.96, Dizeli inapanda kwa Ksh.21.32, huku Mafuta ya Taa yakipanda juu zaidi kwa Ksh.33.13 kwa lita.