logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wenye hatia wanaogopa, Karua asema baada ya 'Chebukati Three' kupuuza wito wa timu ya mazungumzo

Watatu hao walisema kushiriki mazungumzo hayo kutakuwa kuunga mkono uvunjaji wa sheria.

image
na Davis Ojiambo

Habari29 September 2023 - 06:47

Muhtasari


  • • Chebukati alieleza kuwa tume hiyo inafaa kuundwa ili kuchunguza matukio yasiyopendeza ya Agosti 15, 2022, katika eneo la Bomas of Kenya ambayo kulingana naye yaliletea Kenya sifa mbaya.

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua amejibu baada ya waliokuwa Makamishna wa IEBC maarufu kama 'Chebukati three' kukosa kufika kuwasilisha maoni yao kwa Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano (NADCO).

Watatu hao ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, na makamishna wa zamani Abdi Guliye na Boya Molu.

Katika majibu yake, Karua alisisitiza kwamba walishindwa kufika mbele ya kamati ya mazungumzo kwa sababu walikuwa na hatia na hivyo wanaogopa.

"Wenye hatia wanaogopa," Karua alisema kwenye tweet.

Walikuwa wamepangwa kufika mbele ya NADCO siku ya Alhamisi mwendo wa saa sita mchana.Watatu hao kwenye taarifa walisema kuwa kushiriki mazungumzo hayo kutakuwa sawa na kuunga mkono uvunjaji wa sheria.

"Hatutafika mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano kujadili masuala ambayo yametatuliwa. Kwa heshima kubwa kwa Kamati, kushiriki kwetu katika mazungumzo hayo kutakuwa usaliti usio na kikomo kwa Wafanyakazi wa IEBC ambao waliteswa na kuuawa," walisema.

"Badala yake iundwe Tume ya Uchunguzi."Waliongeza kuwa baada ya uchunguzi huo adhabu ifaayo itolewe kwa waliohusika.

Chebukati aliangazia kuwa matokeo ya uchunguzi huo yataimarisha uhuru wa IEBC na kuhakikisha kwamba inadumisha hadhi iliyopendekezwa katika Katiba.

Chebukati alieleza kuwa tume hiyo inafaa kuundwa ili kuchunguza matukio yasiyopendeza ya Agosti 15, 2022, katika eneo la Bomas of Kenya ambayo kulingana naye yaliletea Kenya sifa mbaya.

Makamishna wengine wa zamani wakiongozwa na aliyekuwa naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Francis Wanderi na Justus Nyang'aya walifika mbele ya kamati hiyo na kuwasilisha maoni yao.

Katika wasilisho kwa kamati hiyo, ‘Cherera Four’ walisema walilazimika kujiuzulu baada ya kutilia shaka mchakato uliopelekea kutangazwa kwa matokeo ya urais.

Cherera na Masit walitoa mawasilisho yao kwa njia ya video. Walisema walilazimika kutoroka nchini baada ya kupokea vitisho kutokana na misimamo yao.

Makamishna hao wanne walikataa matokeo ya urais yaliyotangazwa na Chebukati mnamo Agosti 15, 2022, wakidai ujumlishaji wa mwisho wa matokeo ulikumbwa na hitilafu na dosari.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved