logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Uvumi wa kuwepo kwa makaburi na mochwari kwa kanisa la Pasta Ezekiel ni uongo - seneti

Leo Jumanne ni zamu ya Mackenzi na Johansen Oduor kufika mbele ya kamati hiyo.

image
na Davis Ojiambo

Habari17 October 2023 - 05:35

Muhtasari


  • • Alitetea mali yake na shughuli zake za kanisa, akisema kwamba zilifadhiliwa na matoleo ya washarika wake zaidi ya 45,000.
Pasta Ezekiel

Kamati ya muda ya Seneti ambayo imekuwa ikilivalia njuga suala la mauaji ya halaika katika shamba la Shakahola yanayowahusisha wachungaji Mackenzi na Ezekiel imepuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa makafani na makaburi katika kituo cha New Life Prayer Centre na Kanisa la Mavueni, Kaunti ya Kilifi, ambako Kasisi Ezekiel Odero anaendesha huduma yake.

Kamati hiyo, ikiongozwa na Seneta wa Tana River, Danson Mungatana, ilizuru majengo ya kanisa hilo mnamo Jumatatu, Oktoba 16, kama sehemu ya ujumbe wao wa kutafuta ukweli kuhusu madai ya mafunzo ya itikadi hasi na mauaji ya halaiki ambayo yametolewa dhidi ya Odero na kanisa lake.

“Tuliambiwa kuna chumba cha kuhifadhia maiti na makaburi hapa. Hatujaona chumba cha kuhifadhia maiti wala kaburi tunapoendelea na uchunguzi wetu,” alisema Mungatana.

Odero, ambaye anahusishwa na mauaji ya Shakahola yaliyogharimu maisha ya zaidi ya 400 katika Kaunti ya Kilifi, alikana kuhusika na mauaji hayo na kujitenga na mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie, ambaye ndiye mshukiwa mkuu katika kesi hiyo.

Pia alisema kuwa nyumba inayodaiwa kuwa chumba cha kuhifadhia maiti kwa hakika ilikuwa chumba cha usambazaji umeme na udhibiti wa kanisa.

"Hifadhi ya maiti inayodaiwa ni usambazaji wa nguvu za umeme kwa majengo ya kanisa. Hapa ndipo vyombo vya habari vilipodai kuwa kulikuwa na chumba cha kuhifadhia maiti. Ikiwa kuna nyingine ningependa kuwaonyesha,” alisema Odero.

Alitetea mali yake na shughuli zake za kanisa, akisema kwamba zilifadhiliwa na matoleo ya washarika wake zaidi ya 45,000.

Alisema kanisa lake limejenga bwawa la kuogelea la kisasa, maabara yenye vifaa vya kutosha na uwanja wa michezo katika Kaunti ya Kilifi.

Pia alikashifu kile alichokitaja kuwa lawama tupu kwa wahubiri nchini Kenya, akiitaka Serikali kuwaadhibu wachungaji walaghai.

Jumanne leo itakuwa ni zamu ya mhubiri tata Paul Mackenzi na mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor kufika mbele ya kamati hiyo ya seneti.

Oduor alitakiwa kujiwasilisha mbele ya kamati hiyo baada ya kukataa kutokea kwa mara kadhaa, hatua iliyoipelekea kamati hiyo kumpiga faini ya shilingi laki 5.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved