Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Kerio Valley Development Authority, KVDA Silvenus Tubei aliyetoweka Septemba 2012 amepatikana amezikwa mita chache tu kutoka kwa ua la nyumba yake huko kaunti ndogo ya Keiyo Kusini kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Mpaka kutoweka kwake kwa njia ya utatanishi asubuhi ya Septemba 26, 2012, Tubei alikuwa mkurugenzi mtendaji wa KVDA na juhudi za kumtafuta zilifeli kuzaa matunda baada ya msako wa siku kadhaa na familia lakini pia na vyombo vya dola.
Mabaki ambayo yalifunikwa katika blanketi yaligunduliwa yakiwa yamezikwa kwenye kaburi lenye kina kifupi mita chache kutoka kwenye nyumba yake ya kifahari kando ya bustani ya cha maua.
Zoezi la uchimbaji wa kaburi kwa sasa linafanywa na wapelelezi wa mauaji kutoka Kurugenzi ya Uchunguzi wa Jinai DCI.
Tubei alitoweka nyumbani kwake katika kijiji cha Kabiemit, Chepkurmum, eneo la Tumeiyo katika kaunti ndogo ya Keiyo kusini, asubuhi ya Septemba 26, 2012.
Mtunza bustani alijikwaa kwenye blanketi lililozikwa wakati akijaribu kuchimba kutoka kwa ardhi na kugundua mifupa ya binadamu mzima.
Kulingana na OCPD wa Keiyo kusini Abdullahi Dahir Wachunguzi wangetafuta DNA kuthibitisha ikiwa inalingana na ile ya Tubei na kubaini mazingira ambayo alipoteza maisha.
Tubei alisimamia ujenzi wa Bwawa la Turkwel la mabilioni ya dola, ambapo KVDA ilikuwa wakala wa utekelezaji, na ujenzi wa makao makuu ya shirika la KVDA yenye orofa 14 huko Eldoret.