Mwimbaji wa nyimbo za Injili wa Afrika Kusini Kelly Khumalo aliamuru kuuawa kwa mpenzi wake wa wakati huo, nyota wa kandanda Senzo Meyiwa, mahakama imeambiwa.
Bw Meyiwa alipigwa risasi akijaribu kumlinda Bi Khumalo dhidi ya majambazi waliojihami mwaka wa 2014. Washukiwa watano walikamatwa mwaka wa 2020.
Mpelelezi mkuu Bongani Gininda aliiambia Mahakama Kuu ya Gauteng, Jumatano, Bi Khumalo alipanga "mauaji".
Msemaji wa Bi Khumalo aliambia BBC kwamba "wanaamini mchakato wa kisheria".
Waliongeza kuwa Bi Khumalo hakuweza kutoa maoni yake lakini "timu yake ya kisheria inashughulikia kikamilifu hali hiyo".
Kesi ya wanaotuhumiwa kumuua Bw Meyiwa, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya soka na kipa wa Orlando Pirates, imeshika kasi nchini.
Bi Khumalo alishukiwa kwa mara ya kwanza kuhusika baada ya stakabadhi za polisi kuvuja mwaka wa 2020 kufuatia kukamatwa kwa watu hao.
Wakati huo wakili wake aliambia vyombo vya habari vya ndani mwimbaji huyo "hakuwafahamu" watu hao watano.
Bw Gininda aliambia mahakama, mmoja wa washukiwa alisema katika maelezo yake ya kukiri kwamba Bi Khumalo alikuwa amewapa maagizo ya kumuua Bw Meyiwa.
Mpelelezi mkuu pia alisema Bi Khumalo aliunganishwa na washukiwa kupitia "mawasiliano ya simu za rununu".
Mbali na hayo, Bi Khumalo pia alikuwa na picha ya pesa kwenye begi yenye uwazi kwenye simu yake - picha hiyo hiyo ilipatikana kwenye simu moja ya mshukiwa.
Kwa sasa mahakama inathibitisha iwapo taarifa za kukiri kosa zinakubalika. Washukiwa wawili wanasema kukiri kwao kulifanywa kwa kulazimishwa.
Bi Khumalo na Bw Meyiwa walikuwa na mtoto mmoja pamoja.
Lakini Bw Gininda alisema wawili hao walikuwa wametofautiana.
Alisema Bi Khumalo "alimchukia na alitaka kumuondoa".
Aliongeza kuwa "rekodi za mawasiliano" kati ya Bi Khumalo na dadake kutoka mapema 2013 zilionyesha kuwa alitaka kumfukuza kazi.