Ripoti ya Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeweka wazi ukiukaji wa kutisha unaofanywa na pande zote mbili katika vita nchini Sudan.
Ripoti hiyo inahusu miezi minane baada ya mzozo huo kuzuka mwezi wa Aprili mwaka jana na ina ushahidi kutoka kwa mamia ya watu.
Inapendekeza maelfu ya watu wameuawa katika mashambulizi ya kikabila katika eneo la Darfur na inajumuisha madai ya watoto kubakwa.
Picha za satelaiti zinaonyesha kuenea kwa matumizi ya vilipuzi vizito kwenye maeneo yenye watu wengi, na kuua idadi kubwa ya raia.
Ripoti hiyo inajiri baada ya kanda za video kuibuka wiki hii za wanafunzi wakikatwa vichwa na wanaume waliovalia sare ambao baadaye waliviweka vichwa vilivyokatwa kwenye vijiti barabarani.
Umoja wa Mataifa unatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na mazungumzo jumuishi kuelekea serikali ya kiraia nchini Sudan.