logo

NOW ON AIR

Listen in Live

'Nani ataniita Baba?' Kilio cha baba wa Gaza aliyepoteza jamaa 103

Ahmad al-Ghuferi alinusurika kuuawa na bomu lililoiangamiza familia yake.

image
na Davis Ojiambo

Habari27 February 2024 - 04:57

Muhtasari


  • • Ahmad alikuwa akifanya kazi katika eneo la ujenzi la Tel Aviv wakati Hamas iliposhambulia Israel tarehe 7 Oktoba.
Ahmad al-Ghuferi alikwama katika Ukingo wa Magharibi wakati bomu lilipoua watu 103 wa familia yake katika mji wa Gaza.

Ahmad al-Ghuferi alinusurika kuuawa na bomu lililoiangamiza familia yake.

Wakati jamaa 103 walipouawa katika shambulio kwenye nyumba ya familia yao katika jiji la Gaza, alikuwa amekwama maili 50 (80km) kutoka, katika mji unaokaliwa wa Ukingo wa Magharibi wa Jericho.

Ahmad alikuwa akifanya kazi katika eneo la ujenzi la Tel Aviv wakati Hamas iliposhambulia Israel tarehe 7 Oktoba - hakuweza kurudi kwa mke wake na binti zake watatu kwa sababu ya vita vilivyofuata, na vizuizi vya jeshi la Israel.

Alizungumza nao kwa wakati mmoja kila siku, wakati mtandao wa mawasiliano ya simu iliporuhusu, na alikuwa akizungumza na mkewe, Shireen, wakati kwa simu shambulio lilipotokea jioni ya 8 Desemba.

"Alijua atakufa," alisema. "Aliniambia nimsamehe kwa lolote baya ambalo huenda alinifanyia. Nilimwambia hakuna haja ya kusema hivyo. Na hiyo ndiyo ilikuwa simu ya mwisho kati yetu."

Shambulio kubwa la bomu dhidi ya nyumba ya mjomba wake jioni hiyo lilimuua mkewe na binti zake watatu wachanga - Tala, Lana na Najla.

Pia ilimuua mama yake Ahmad, ndugu zake wanne na familia zao, pamoja na makumi ya shangazi zake, wajomba zake na binamu zake. Zaidi ya 100 walikufa kwa jumla. Zaidi ya miezi miwili baadaye, baadhi ya miili yao bado imenaswa chini ya vifusi.

Wiki iliyopita, aliadhimisha siku ya kuzaliwa ya bintiye mdogo - Najla ambaye angetimiza miaka miwili. Ahmad bado anajaribu kufahamu kilichotokea.

Hakuweza kushikilia miili ya watoto wake au kuwa katika mazishi yao ya haraka, bado anazungumza juu yao katika wakati uliopo, uso wake unabubujikwa machozi.

"Binti zangu ni ndege wadogo kwangu," alisema. "Ninahisi niko ndotoni. Bado siamini kilichotutendekea'

Ameondoa picha za wasichana hao kwenye skrini ya simu na kompyuta yake ya pajani, ili asikutane nazo.

Ameachwa kuelewa kile kilichotokea kutoka kwa simulizi za jamaa na majirani wachache waliobaki.

Walimwambia kwamba kombora kwanza lilipiga mlango wa nyumba ya familia yake.

"Walitoka haraka na kwenda nyumbani kwa mjomba wangu karibu," alisema. "Dakika kumi na tano baadaye, ndege ya kivita ilishambulia nyumba nyumba hiyo."

Jengo la ghorofa nne ambako familia hiyo iliuawa lilikuwa pembeni mwa Kituo cha Matibabu cha Sahaba katika kitongoji cha Zeitoun katika Jiji la Gaza.

Sasa ni kifusi cha saruji iliyopasuliwa; kikombe cha plastiki cha kijani kibichi, mapande ya nguo zenye vumbi vimetapakaa.

Fremu iliyokunjwa ya gari la rangi ya fedha, kioo chake cha mbele kilichopinda na kuwa giza, kiko karibu na mawe ya zege yanayoning'inia.

Mmoja wa jamaa za Ahmad aliyenusurika, Hamid al-Ghuferi, aliambia BBC kwamba wakati shambulio hilo lilipoanza , wale waliokimbia juu ya mlima huo walinusurika, na wale waliokimbia kutafuta hifadhi katika nyumba hiyo waliuawa.

"Ilikuwa mkanda wa moto," alisema. "Kulikuwa na shambulio kwenye nyumba nne zilizo karibu na yetu. Walikuwa wakishambulia nyumba kila baada ya dakika 10."

"Watu 110 kutoka kwa familia ya Ghuferi walikuwepo - watoto wetu na jamaa," alisema. "Wote isipokuwa wachache waliuawa."

Walionusurika wanasema mwathiriwa mkubwa alikuwa nyanya mwenye umri wa miaka 98; mtoto mdogo wa kiume aliyezaliwa siku tisa tu mapema.

Jamaa mwingine, binamu ambaye pia anaitwa Ahmad, alielezea milipuko miwili mikubwa ya shambulio la anga.

"Hakukuwa na onyo la mapema," alisema. "Kama watu [baadhi] hawakuwa tayari wameondoka eneo hili, nadhani mamia wangeuawa. Eneo hilo linaonekana tofauti kabisa sasa. Kulikuwa na maegesho ya magari, mahali pa kuhifadhi maji, na nyumba tatu pamoja na nyumba moja kubwa, mlipuko huo uliharibu eneo lote la makazi."

Hamid alisema walionusurika walifanya kazi hadi asubuhi na mapema ili kuopoa miili hiyo kutoka kwenye vifusi.

"Ndege zilikuwa zikielea angani, na zilikuwa zikiturushia risasi tulipokuwa tukijaribu kuzitoa," binamu Ahmad alisema.

"Tulikuwa tumekaa ndani ya nyumba na tukajikuta chini ya vifusi," Umm Ahmad al-Ghuferi aliambia BBC. "Nilitupwa kutoka upande mmoja hadi mwingine. Sijui walinitoaje. Tuliona kifo mbele ya macho yetu."

Miezi miwili na nusu baadaye, bado wanajaribu kufikia baadhi ya miili iliyofukiwa chini ya vifusi. Familia hiyo imekusanya pesa ili kukodi ndogo kufukua vifusi.

"Tuliokota miili minne [leo]," Ahmad aliiambia BBC, "ikiwa ni pamoja na mke wa kaka yangu na mpwa wangu Mohammed, ambaye alitolewa vipande vipande. Walikuwa wamekaa chini ya vifusi kwa siku 75."

Makaburi yao ya muda yapo kwenye kipande cha ardhi tupu kilicho karibu, kilicho na vijiti na karatasi za plastiki.

Ahmad, aliyekwama Jericho, hajawatembelea.

"Nilifanya nini hadi kupokonywa mama yangu, mke wangu, watoto wangu na kaka zangu?" Aliuliza. "Wote walikuwa raia."

Tuliuliza jeshi la Israel kuhusu madai ya familia hiyo kwamba ililengwa na mashambulizi ya anga. Katika majibu yake, jeshi lilisema halijui kuhusu shambulio hilo , na kwamba Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lilichukua "tahadhari zinazowezekana ili kupunguza madhara ya raia" katika vita vyake na Hamas.

Kulikuwa na mapigano makali kati ya vikosi vya Israel na watu wenye silaha wa Hamas katika eneo la Shejaiyya, kusini mwa nyumba ya al-Ghuferi, katika siku chache kabla na baada ya familia ya Ahmad kuuawa.

Katika taarifa ya kila siku ya tarehe 9 Disemba, jeshi lilisema kuwa "liliwatambua magaidi kadhaa waliokuwa na makombora ya kulenga vifaru" wakiwakaribia wanajeshi huko Shejaiyya, na kuitisha shambulio la helikopta dhidi yao.

Pia ilisema ndege za kivita zilikuwa zikishambulia maeneo ya ugaidi katika Ukanda wa Gaza, huku operesheni za ardhini zikiendelea.

Eneo la Zeitoun, ambapo nyumba ya familia iliwahi kuwa, sasa ni kitovu cha shughuli mpya za IDF.

Huko Jericho, Ahmad bado wakati mwingine huwapigia simu jamaa zake waliosalia huko Gaza. Lakini baada ya miezi kadhaa ya kunaswa nje ya nyumba yake anayoipenda na kukata tamaa ya kurudi, hana uhakika kama atarudi tena.

"Ndoto yangu ilivunjwa huko Gaza," alisema. "Nirudi kwa nani? Nani ataniita baba? Nani ataniita mpenzi? Mke wangu alikuwa akiniambia mimi ndiye maisha yake. Nani ataniambia hivyo sasa?"


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved