Mamlaka nchini Kenya imeanza kuachilia mabaki ya watu waliofariki katika ibada inayodaiwa kuwahamasisha kufunga hadi kufa kwa njaa.
Miili 34 kati ya 429 ilifukuliwa katika msitu wa Shakahola karibu na mji wa Malindi pwani yaKenya imetambuliwa kwa msaada wa sampuli za DNA kutoka kwa jamaa zao.
Siku ya Jumanne miili saba ilikabidhiwa kwa familia tatu.
Mchungaji Paul Nthenge Mackenzie aliyetoa mahubiri kwamba nyakati za mwisho zimekaribia, anashtakiwa kwa kuchochea mamia ya wafuasi wake “kufunga” ili kumwona Yesu, jambo ambalo anakanusha.
Mwalimu wa shule ya upili Francis Wanje alipokea miili minne, ikiwa ni pamoja na ya bintiye, mkwe wake na mjukuu wake.
Alipoteza watu wanane wa familia yake, na kutoweka kwao ndiko kulikosaidia wachunguzi kugundua makaburi ya halaiki katika msitu huo mkubwa.
Jamaa walipewa ushauri wa kisaikolojia na wanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.
Wafanyakazi wa ICRC pia waliwaunga mkono baadhi yao huku wakiomboleza na kulia walipopelekwa kutazama mabaki ya wapendwa wao.
Mchakato wa uchungu wa utambuzi umechukua mwaka, kwa sababu miili mingi ilikuwa imeharibika vibaya, kulikuwa na idadi kubwa ya kesi, na hakuna kitendanishi cha kutosha na vifaa vya kufanya vipimo vyote vya DNA
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya imechukizwa na ucheleweshaji huo.
Lakini mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor alisema wiki jana kwamba familia nyingi hazikuwa zikija kudai miili hiyo, na hivyo kufanya kuwa changamoto kupata sampuli za DNA.
Pia kuna suala la gharama. Mwana na kaka wa mmoja wa marehemu walisafiri kwa basi kutoka kaunti moja Magharibi mwa Kenya na hawakuwa na uwezo wa kusafirisha mwili nyumbani.
Wanaomba msaada, lakini serikali imesema familia zinatakiwa kuandaa mazishi ya wafu wao.
Mwezi uliopita Mackenzie na washtakiwa wengine 29 walishtakiwa kwa makosa kadhaa yakiwemo ya mauaji ya watoto 191. Walikanusha mashtaka hayo.