Idara ya utabiri wa Hali ya Hewa nchini imetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa mvua kubwa kuanzia Ijumaa na kundelea wikendi yote.
Katika taarifa siku ya Alhamisi, Mkurugenzi wa Idara hiyo David Gikungu alisema mvua kubwa inatarajiwa kushuhudiwa katika jumla ya kaunti 46 maeneo kama vile Bonde la Ufa, Nairobi, Bonde la Ziwa Victoria na Pwani.
Gikunga alisema mvua hiyo ambayo hadi sasa imesababisha vifo kadhaa na hasara kubwa itaongezeka kwa siku mbili na kupungua siku ya Jumapili.
Athari za mvua inayoendelea kunya zimeshuhudiwa katika maeneo mengi ya nchi huku barabara zikigeuka kuwa mito katika mji mkuu wa Nairobi.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu 32 wamepoteza maisha na zaidi ya 40,000 wakilazimika kuyahama makazi yao kutokana na mvua na mafuriko.
Jumatano asubuhi, Shirika la Reli la Kenya lilisema mafuriko hayo yameathiri njia za reli, na hivyo kufanya kuwa vigumu kwa treni kufanya kazi.
Kampuni hiyo ilisema hofu ya usalama iliilazimisha kusitisha huduma zake.