Polisi kwa ushirikiano na bodi ya utumishi wa umma katika kaunti ya Migori, wamemtia mbaroni mshukiwa mmoja wa mwenye umri wa makamu wa kiume kwa madai ya ulaghai na utapeli wa kujifanya mmojawapo wa wanachama wa bodi hiyo ya utumishi wa umma wa kaunti ya Migori.
Inasemekana kuwa, mshukiwa huyo alikuwa anajishirikisha katika tuhuma ya ulaghai kwa minajili ya kuwaibia wananchi waliokuwa kwenye pilkapilka za kutafuta kazi kwenye kaunti ya Migori.
Kulingana na Andrew Okatch, Afisa Mkuu Mtendaji wa bodi ya utumishi wa umma katika kaunti ya Migori, mshukiwa alikamatwa katika kituo cha uchukuzi na biashara cha Masara kwenye gatuzi ndogo ya Suna Magharibi.
Maafisa wa polisi wamekuwa kwenye pilkapilka za kumsaka kwa muda mpaka pale walipo mtia mbaroni.
Fauka ya hayo, Okatch aling’amua kuwa mshukiwa yumo korokoroni ambapo anangojewa kujibu mashtaka ya madai dhidi yake yanayomkabili.
Vilevile, Okatch alisema kuwa, mmojawapo ya waja waliotapeliwa alishaandikisha taarifa kwa kituo cha polisi.
Okatch pia, alisema kuwa aliandikisha taarifa ya ujumbe wa utapeli kwa kituo cha kurekebisha maadili kwa niaba ya bodi na wanachama wote waliohusishwa kwenye mzozo huo .
Afisa huyo mkuu mtendaji wa bodi ya utumishi wa umma kaunti ya Migori,vilevile, amewatahadharisha wananchi wa kaunti ya Migori wachukue tahadhari na umakini hasa wanapojishiriksha na shughuli za kutafuta kazi wasije wakajutia kwa kwikwi na simanzi wanaponaswa na mtego huu mzito wa utapeli.