Mtu mmoja katika kaunti ya Kakamega eneo bunge la Mumias Mashariki amefariki kufuatia kupigwa na radi masaa ya jioni.
Mwanamume huyo mwenye umri wa makamu inasemekana kwamba, alikuwa nyumbani kwake eneo la Eshilarumwa wakati mkasa huo ulipomfika na kumfisha.
Ripoti zaidi, vilevile, zinaashiria kuwa mkasa huo ulimfika masaa ya jioni mnamo 7.30 pm ya Jumanne.
Marehemu, Rashid Ondewa, alikuwa amesimama kando ya jikoni wakati radi ilimfika na kumfisha kwa mujibu wa jamaa yake Tahiri Omumasaba.
Juhudi na jitihada za kumfikisha zahanatini ziliambulia patupu kwani Ondewa alifariki kwenye shughuli na pilkapilka za kumfikisha hospitalini na kuokolewa. Waama, mkono mtupu haurambwi.
“Ameondoka na kuacha pengo kubwa isillojazilika katika familia yetu. Rashid alikuwa nguzo adhimu katika familia yetu,” aliongeza Omumasaba huku akizungumza na Citizen.
Wafanyibiashara wenza wa soko la Shianda ambapo marehemu alikuwa akifanya kazi walimkumbuka marehemu kama mfanyibiashara mwenye bidii na ukakamavu wa kuigwa na kupigiwa mfano.
Mola ailaze roho yake mahali pema peponi na vilevile aifariji familia, jamaa na marafiki.