logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mbunge Racheal Nyamai Akosoa Maandamano ya Gen Z

Racheal Nyamai amewashtumu vijana wa Gen Z kutokana na maandamano akidai wengi wanatafuta tu umaarufu Tiktok.

image
na Davis Ojiambo

Habari20 June 2024 - 09:44

Muhtasari


  • •Racheal Nyamai amedai kuwa vijana wa Gen Z wanajihusisha tu kwa maandamano ili kupata umaarufu kwenye mtandao wa Tiktok.
  • •Hatma ya mswada wa fedha 2024 itafahamika leo Juni 20 baada ya wabunge kupiga kura.
Mbunge wa Kitui Kusini

Mbunge wa Kitui Kusini Racheal Nyamai amedai kuwa maandamano ya vijana dhidi ya mswada wa fedha 2024 jijini Nairobi hayachochewi na nia nzuri, bali kupata tu umaarufu  Tiktok.

Nyamai alisema hayo alipokuwa akijadili muswada wa sheria ya fedha bungeni Jumatano Juni 19, 2024. Mbunge huyo alisema baada ya kushiriki maandamano hayo, mmoja wa wanafunzi anaowafadhili shuleni, alitoa maoni yake kwake.

Nyamai alidai kuwa mwanafunzi huyo alimtumia ujumbe mfupi wa simu kueleza wasiwasi wake kuhusu mswada wa fedha, haswa ushuru uliopendekezwa wa usambazaji wa chakula na magari.

Aidha, mbunge huyo alidokeza kuwa mwanafunzi wake aliyemfadhili hakuwa na sababu ya kuendelea kuandamana kwa sababu ushuru kwa upande wa chakula na magari ulikuwa umeondolewa.

"Nilimuuliza kwa nini alikuwa mtaani, na msichana akaniambia kuwa hayupo mtaani kuhusu mswada wa fedha, akaniambia alikuwa huko kwa sababu ya Tiktok..." Nyamai alisema.

Mbunge huyo pia aliendelea kutaja jinsi aliunga mkono mswada huo baada ya sheria ya fedha ya 2023 kufanikiwa. Pia alieleza kuwa sera za serikali zilizowekwa ziliwajibika kwa ukuaji wa uchumi wa Kenya.

Vile vile alidai kuwa kwa kutunga hatua zilizojumuishwa katika mswada wa fedha, ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ungehimiza ukuaji wa wazalishaji wa Kenya. Hii inakuja  baada ya vijana  kumiminika barabarani,wakitaka mswada wa fedha kutupiliwa mbali wengi wakidai kuwa ni kukandamiza wakenya.

Mswada wa fedha 2024,unazidi kupamba moto huku baadhi ya wabunge kama vile Robert Mbui kutoka Kathiani wakipinga,mbunge wa Mugirango Kusini,Silvanus Osoro akiunga mkono.

Hatma ya mswada wa fedha itabainika leo Juni 20 baada ya wabunge kupiga kura bungeni.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved